Archives for News & Events

Waziri Biteko, Prof.Msanjila Wautaka Mgodi Wa North Mara Kutii Mamlaka Za Serikali.

Na. Nuru Mwasampeta

Waziri wa madini Doto Biteko pamoja katibu Mkuu Madini Prof. Simon Msanjila  wakutana na uongozi wa  mgodi wa North Mara  na kuutaka kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika tarehe 17 Januari, 2019 katika ofisi ya waziri jijini Dodoma, Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa walipaswa kuwa wamechukua hatua kadhaa kuonesha kua wanatii maagizo ya Serikali lakini kutokana na wao kuhisi serikali haina cha kufanya wakaamua kutulia kwa miezi mine ambapo wamefika ofisini kueleza masuala ambayo hayajafanyiwa kazi.

“Hatuwezi kuwa tunakaa, tunafikia maamuzi ninyi mnayapinga, ni nani yupo juu ya Serikali” Waziri Biteko alihoji. “Mnajua suala la ardhi ni kubwa sana, mnajua ni maelekezo ya Rais, sasa Rais ameagiza halafu hakitokei kitu! Mimi sielewi kabisa. Afadhali watu wangeanza kulipwa unaweza sema sasa hatua za malipo zinafanyika”alikazia.

Sambamba na hilo Biteko aliwaeleza wajumbe hao kuwa uongozi wa mgodi huo hawamfuati mtu mahususi katika kutatua suala hilo na kubainisha kuwa mgogoro huo hautatatuliwa na wizara ya Madini isipokuwa ni watu wenye mamlaka na masuala ya ardhi.

Akizungumzia chanzo cha mgogoro kuchukua muda mrefu Biteko alieleza kuwa tatizo la kuongezeka gharama za malipo kumetokana na mgodi kuchelewesha malipo ya tathimini ya awali ambayo ilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6, hii imepelekea kufanyika kwa tathimini ya pili iliyopelekea kufikia kiasi kikubwa cha bilioni 12 ukilinganisha na kile cha awali.

Hii ni kutokana kwamba, mara baada ya tathmini kufanywa kwa ajili ya malipo ya fidia, malipo yanapaswa kufanyika si zaidi ya miezi sita na baada tu ya tathmini kufanyika; aidha, mgodi ulipaswa kutoa tangazo ili kusimamisha uendelezaji wa maeneo kwani maeneo yakiendelezwa na tathmini kutolipwa kwa wakati kiasi kilichothaminishwa awali kinakuwa si dhahiri tena maana  uwekezaji katika eneo husika unaongezeka.

Akifafanua hilo mara baada ya kuzungumza na mthaminishaji Mkuu wa Serikali kwa njia ya simu, Biteko alisema ameelezwa kwamba tathmini inayofuatwa ni ile iliyofanyika awamu ya pili maana hiyo ndiyo ya sasa na kukazia kuwa hawawezi kufuata ya awali kutokana na kwamba muda wa kuwalipa fidia hizo ulipaswa kutozidi miezi sita tangu tathmini kufanyika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Madini Prof Simon Msanjila alisema haiwezekani aje mtu asiyekuwa na maamuzi, Waziri atoe maamuzi halafu mtu aliyeko Uingereza ayapinge huu ni udhalilishaji, maamuzi ya mwisho yakishafanyinywa na Serikali hakuna serikali nyingine au kampuni iyapinge! Maamuzi yanayotolewa Tanzania hayawezi kwenda kujadiliwa London sio Sheria hiyo, ndio maana kampuni lazima iwe imesajiliwa Brella, kwa hiyo hakuna mambo ya kusema mshauri yupo London, South Africa. Alisisitiza.

Msanjila aliwakumbusha kuwa makubaliano waliyoafikiana katika vikao vya nyuma kuwa endapo kiongozi yeyote wa North Mara anafahamu kuwa hana mamlaka ya kufanya maamuzi asihudhurie katika vikao vinavyolenga kupitisha maamuzi yazingatiwe.

Alipojaribu kujibu hoja hizo Bi Jane Reuben Lekashingo ambaye ni mmoja wa viongozi kutoka mgodi wa North Mara alisema kuwa kiongozi mkuu wa masuala ya kisheria katika mgodi huo yupo nchini Uingereza na kwamba endapo kunakuwa na suala lolote la kisheria ni sharti ashirikishwe ili kufanya maamuzi ya pamoja. Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila alihoji endapo north Mara ipo juu ya Serikali?

Prof. Msanjila aliendelea kwa kusema, Huyu ni waziri, anamwakilisha Rais, hamuwezi kwenda kuomba ushauri London kwa maagizo yaliyotolewa na waziri, hiyo si sheria, alikazia.

Don’t talk about London or South Africa tunapoongelea masuala ya Tanzania tunaongea kwa sheria za Tanzania we have nothing to do with London hiyo ni yao” alisisitiza.

Baada ya mahojiano makali na yaliyochukua muda mrefu baadaye viongozi wa mgodi wa North Mara walielewa na kukiri kwamba baadhi ya wananchi waliofanyiwa tathmini ya malipo yako sahihi na kuahidi kufanya malipo, na kuahidi kwamba baada ya kufika katika vituo vyao vya kazi watakwenda kuendelea na taratibu za malipo ili kuonesha uungwana kwamba wamechukua hatua na kuonesha utii kwa mamlaka ya Serikali kwa kutii makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wakuu wa nchi.

Pamoja na kukiri kuwa wamejifunza kitu kutokana na kikao hicho viongozi hao walisema wataendelea kujifunza kwani wameona kuchelewa kwao katika kulipa fidia hizo kumeipelekea kampuni kutakiwa kutumia kiasi kikubwa cha pesa katika kulipa wananchi kutokana na shughuli za kimaendeleo walizoendeleza kuwekeza katika maeneo yao.

Aidha kutokana na uhalisia kisheria kuwa; tathmini ya ardhi ni hai kwa kipindi cha miezi sita na ikizidi hapo inafanyika tathmini nyingine lakini pia wamejifunza juu ya taratibu na sheria za kusitisha shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa kutangaza kusimamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini kwa kipindi cha miezi sita na pia kulipa fidia kwa wakati ili wananchi wakajiendeleze katika maeneo mengine watakayohamia.

Read more

Madini Kufanya Mazungumzo Barabara Mgodi Wa Makaa, Ngaka

Na Asteria Muhozya, Mbinga

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema Wizara yake itafanya mazungumzo na  Mamlaka zinazohusika na masuala  ya barabara ili kuweka mazingira bora ya miundombinu hiyo  kwa lengo la  kuwezesha biashara ya makaa ya mawe na shughuli za uzalishaji makaa hayo kufanyika kwa ufanisi zaidi katika mgodi wa makaa ya mawe  Ngaka, uliopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.  

Alisema mgodi huo wa Ngaka chini ya kampuni ya TANCOAL ndiyo taswira ya uzalishaji makaa ya mawe nchini hivyo, serikali haina budi kuweka mazingira bora yatakayowezesha kupunguza gharama za uendeshaji jambo ambalo litapunguza gharama kwa walaji wa nje na ndani ikizingatiwa kuwa, ni kampuni ya Kimataifa kutokana na kuhudumia wateja kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Uganda nchi na nyingine.

Kauli ya Naibu Waziri Nyongo inafuatia changamoto ya barabara iliyowasilishwa kwake na Meneja Mgodi wa TANCOAL Mhandisi David Kamenya, ambaye alimweleza Naibu Waziri kuwa, ukosefu wa miundombinu imara ikiwemo madaraja imechangia shughuli za upakiaji makaa hayo kutokuzidi tani 20 kwa kila gari jambo ambalo linapelekea kuwepo na foleni kubwa  kutokana na uhitaji wa makaa hayo.

Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara mgodini hapo Januari 17 ikilenga kukagua shughuli za madini mkoani Ruvuma pamoja na kuangalia changamoto mbalimbali ambazo mgodi huo unakabiliana nazo katika utekelezaji wa shughuli zake.

Pamoja na kuridhia ombi hilo, Naibu Waziri aliitaka kampuni hiyo kuongeza kasi ya uzalishaji kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo katika soko la nje na ndani na kuitaka kutobweteka huku ikitakiwa kuboresha huduma inazotoa ikiwemo kuongeza vifaa vya kazi.

“Nimeona changamoto ya barabara. Kama serikali ni lazima tuifanyie kazi changamoto hii ili kuwezesha uzalishaji zaidi wa makaa. Sisi tutaendelea kutoa leseni kwa wazalishaji wengine ili kuweka ushindani, hivyo msibeweteke, tunahitaji sana makaa haya kwa uchumi wa taifa letu kwa kuwa tunayo hazina ya kutosha ya rasilimali hii,” alisema Nyongo.

Aliongeza kuwa, kufuatia serikali kuweka zuio la uingizaji makaa kutoka nje, ni lazima kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa madini hayo ikiwemo kuwezesha biashara hiyo   na kuutaja mgodi wa makaa ya mawe wa Kabulo unaomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwa ni eneo jingine ambalo miundombinu ya barabara ni lazima iboreshwe kuwezesha  ufanisi zaidi wa shughuli za uzalishaji madini hayo.

Alisema kuwa, ili serikali iendelee kupata mrabaha zaidi kutokana na rasilimali hiyo suala hilo lazima lichukuliwe kwa uzito ili kuongeza mapato zaidi.

Sehemu ya Mgodi wa Makaa ya mawe, Ngaka.

Aidha, akijibu ombi la kampuni hiyo kutaka kurudishiwa eneo ambalo lilitolewa kwa ajili ya Kiwanda cha Dangote na Rais John Magufuli, kwa kuwa bado haijanza kuchimba mpaka sasa, Naibu Waziri Nyongo alizitaka pande zote ikiwemo wizara na kampuni hizo kukutana Januari 22 mara baada ya kikao cha wadau wa sekta ya madini ili kujadili suala hilo ili hatimaye shughuli za uzalishaji zianze katika eneo hilo.

Mbali na hilo, kampuni hiyo ilimwomba Naibu Waziri kuwezesha upatikanaji wa leseni mbili zilizoombwa na kampuni hiyo ikilenga kutumia makaa hayo kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya mgodi. Naibu Waziri aliahidi kuwa, kupitia Tume ya Madini, suala hilo litakuwa limekamilika ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliitaka Halmashauri ya Mbinga kubuni miradi kwa ajili ya vijana na wanawake yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kuachana na matumizi ya mkaa kwa kuwa umekuwa ukisababisha uharibifu wa mazingira.

Wakati huo huo, akizungumzia suala la Mrabaha wa serikali  wa asilimia 3, alisema usilipwe kwa bei ya maeneo ya uchimbaji   bali ulipwe kwa bei ya sokoni. Hivyo, aliwataka wazalishaji wote na Maafisa wa Tume ya Madini kuhakikisha wanatoza bei ya sokoni na siyo ya uzalishaji.

Kwa upande wake, Meneja wa  mgodi  Mhandisi  David  Kamenya akizungumzia ubora wa makaa hayo, alisema kuwa, Makaa ya Ngaka yana ubora wa kimataifa  na ndiyo sababu imepelekea kupata wateja wengi kutoka nchi mbalimbali na kuongeza kwamba makaa hayo yana uwezo wa kufanya matumizi mbalimbali na kuongeza kuwa, kwa siku kampuni hiyo inapakia idadi ya magari yapatayo 100.

AKizungumzia malengo ya baaaye, alisema kuwa, idadi ya mashine ndani ya siku chache zinatarajiwa kuongezwa na kwamba kampuni imelenga kuzalisha hadi tani 5,000 kwa siku kutoka 3,000 za sasa.

Akizungumzia uwezeshaji kwa vijana na akina mama, alisema kuwa, tayari kipo kikundi cha wakina Mama cha Mbarawala ambacho kimewezeshwa na  mgodi huo kwa kupatiwa mafunzo  ya namna ya kuandaa makaa hayo maalum kwa matumizi ya majumbani na kuongeza kuwa, hivi karibuni kikundi hicho kimepata  Cheti cha ubora kutoka shirika la Viwango nchini (TBS) jambo ambalo litawezesha kikundi hicho kuuza  makaa yake kwa ajili ya matumizi ya majumbani na hivyo kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na kukatwa miti.

 Pia, Mhandisi Kamenya alimweleza Naibu Waziri Nyongo kuwa, mbali na kupatiwa mafunzo kikundi hicho pia kimepatiwa mashine ambayo inauwezo wa kuzalisha tani mbili za makaa hayo kwa saa.

Akishukuru kwa niaba ya kikundi, Meneja Usimamizi wa Mbarawala, Joyce Haule alisema kuwa,  wanaishukuru kampuni hiyo kwa kuwawezesha na  kwamba kikundi kinalenga kuzalisha tani 10 kwa siku na kuongeza kuwa, hadi sasa tayari kimepata wateja kutoka maeneo mbalimbali zikiwemo nchi za Rwanda ambao  awali walitaka kwanza kikundi hicho  kuwa na cheti cha ubora wa makaa hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Ishenyi alimweleza Naibu Waziri kuwa, kama Wilaya itahakikisha kuwa, inashirikiana na mamlaka zinazohusika kuweka mazingira bora ya kuwezesha mundombinu bora ya barabaraba  ili TANCOAL iweze kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi.

Katika hatua nyingine, akizungumza na Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Prof. Riziki Shemdoe, ofisini kwake Januari 18, Naibu Waziri alimweleza Prof. Shemdoe umuhimu wa kuwezesha miundombinu ya barabra kuelekea katika mgodi huo wa Ngaka.

Pia, Naibu Waziri alimweleza Prof. Riziki kuhusu mipango ya Serikali ya kuwa na vituo kwa ajili ya biashara ya madini na umuhimu wa mikoa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hizo. “Tunataka kuwa na utaratibu wa kuwa na maeneo ya kuuza na kununua madini ili kuwa na utaratibu maalumu,” aliongeza

Kwa upande wake, Prof. Shemdoe alimwomba Naibu Waziri kusaidia upatikanaji wa wawekezaji kwa ajili ya viwanda vya kuchenjua dhahabu mkoani humo na kukumbushia suala la uchimbaji madini katika Mto Muhuwesi.

TANCOAL ni kampuni yenye ubia na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambapo serikali inamiliki hisa kwa asilimia 30.

Read more

Maafisa Madini Watakiwa Kutobagua Migodi

Na Asteria Muhozya, Mbinga

Maafisa Madini nchini wametakiwa kutobagua migodi midogo kwa kuelekeza nguvu kwenye migodi mikubwa tu huku wakisisitizwa kutatua migogoro kwenye maeneo yao ya kazi na kuelezwa kuwa, watakaobainika wakibagua migodi hiyo na kutotatua migogoro wataondolewa kwenye nafasi zao.

Hayo yalibainishwa Januari 17, 2019 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Sapphire wakati wa ziara yake katika kijiji cha Masuguru, Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

 Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara hiyo ikilenga kukagua shughuli za uchimbaji madini wilayani humo pamoja na kusikiliza kero za wachimbaji katika migodi hiyo, ambapo wachimbaji waliwasilisha kero za kutaka kutengewa maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji, bei elekezi za madini ikiwemo kuunganishwa na huduma ya umeme kwenye migodi yao.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akisamiliana na baadhi ya wachimbaji wa madini ya Sapphire katika kijiji cha Masuguru mara baada ya kuwasili kijijini hap wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini wilayani humo.

Akizungumza kijijini hapo, alimtaka Afisa Madini mkoa wa Ruvuma hukakikisha anaishughulikia kero hiyo na kuitatua mara moja na kuongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano anataka wachimbaji nchini wachimbe madini, hivyo, maafisa madini   kote nchini wahakikishe wanashughulikia kero katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kusuluhisha migogoro.

“Sisi ni matajiri, tumebarikiwa madini ya vito. Wachimbaji chimbeni lakini mchimbe katika maeneo yaliyoruhusiwa kuchimbwa”.alisisitiza.

Alisema kuwa, kama mgogoro ni mkubwa wapo viongozi wa vyama vya wachimbaji wahakikishe kuwa  wanafikisha migororo hiyo na kusema “tuleteeni na sisi lakini  usipoishughulikia migogoro hiyo tutakuondoa.

Aliongeza kwamba, serikali inalenga katika kuwatoa wachimbaji wadogo kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa  kati na hatimaye mkubwa na ndiyo sababu inaendelea na ujenzi wa vituo vya umahiri  katika maeneo mbalimbali nchini ikilenga katika kutoa elimu ya uchimbaji bora, uchenjuaji bora, biashara ya madini na ujasiliamali ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanakua.

Mmoja wa wachimbaji wananwake katika kijiji cha Masuguru akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Ishenyi ( hawapo pichani) wakati wa ziara ya viongozi hao kijijini hapo.

Aliongeza kuwa, elimu ya ujasiliamali ni muhimu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa itawaandaa kuwa na uchimbaji endelevu na wenye tija.

Akijibu ombi la ruzuku,  aliwataka wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi vidogo vidogo  ili iwe rahisi kwa wachimbaji hao kufikiwa  ikiwemo kupatiwa huduma za leseni, elimu, vifaa, kuwamilikisha, kuwapatia mikopo na  kuwafuatilia  jambo ambalo litapelekea wafanye kazi kwa urahisi na kwa kulipa kodi za serikali na  wao kubaki na kipato  kitakachowezesha maisha bora.

Alisema uwepo wa mazingira mazuri migodini utasaidia vijana kufanya kazi na hivyo kuwa na taifa lenye watu wanaofanya kazi.  Aliwataka maafisa madini wote kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya wachimbaji wadogo na kueleza kwamba, endapo serikali itakuta migogogoro ya wachimbaji wadogo  katika maeneo yao wataondolewa.

Aliongeza kwamba, wizara imejipanga na tayari kuna baadhi ya maeneo yametengwa kwa ajili ya wachimbaji  na kuwasisisitiza kuhakikisha wanauza madini  wanayoyachimba katika maeneo rasmi.

Akizungumzia suala la broker, aliwataka kuhakikisha wanakuwa na leseni ya kufanya shughuli hizo ikiwemo vifaa vya kupimia madini na kuwataka kulipa kodi. Pia, aliwatahadharisha wachimbaji wanaoshirikiana na broker wasiokuwa na leseni   kuacha kwani kwa kufanya hivyo ni kwamba wote wanaliibia taifa.” Maafisa madini hakikisheni mnawajua ma broker wote na wawe na leseni na walipe kodi, “alisisitiza Nyongo.

 Akijibu ombi la ruzuku lililowasilishwa kwake, alisema fedha za ruzuku zilizokuwa zikitolewa awali hazikuwafikia walengwa wote na kueleza kuwa, wapo waliopata ruzuku hizo lakini hawakuwa wachimbaji na kuongeza kwamba, hivi sasa wizara inaangalia namna bora ya kuwasaidia wachimbaji.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkoa wa Ruvuma  Abraham  Nkya alisema kuwa, mkoa huo tayari umetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kwamba watashirikiana na wachimbaji hao ili  suala hilo liweze kuwasilishwa Tume ya Madini kwa  ajili ya hatua zaidi.

Awali, kiongozi wa wachimbaji   aliwasilisha ombi kwa Naibu Waziri   la wachimbaji kupatiwa  ruzuku. Alisema mkoa huo umebarikiwa madini ya ujenzi, nishati, viwanda    huku eneo la Masuguru likibariwa madini ya Sapphire. Alisema eneo hilo liliombwa kwa ajjili ya uchimbaji mdogo lakini mpaka sasa bado halijatengwa.

Pia, alisema ipo changamoto ya kukosekana elimu kwa watendaji vijijini ambao wamesababisha mgizo mkubwa wa kodi kwa wachimbaji.

Read more

Madini Kuweka Msukumo Miradi Ya Liganga, Mchuchuma

Na Asteria Muhozya, Ludewa

Wizara ya Madini imesema itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kuweka msukumo ili kuhakikisha kwamba miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Linganga inaanza kutekelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa Januari 16, 2019 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za madini mkoani Njombe na kuona namna ya kutatua changamoto zinazohusu Wizara ya Madini   katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akimsikiliza akimweleza jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake mkoani humo.

Alisema miradi hiyo ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo Taifa linatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa, hivyo kutokana na umuhimu wake, wizara ya madini itashirikiana na wizara hiyo kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili hatimaye miradi hiyo ianze kutekelezwa kwa kuwa imechukua muda mrefu.

Aliongeza kuwa, ni miradi mikubwa ambayo taifa linatarajiwa kunufaika nayo  kupitia ajira  na kuongeza pato la nchi huku akiyataja madini ya chuma kuwa  moja ya malighafi muhimu kwa uchumi  wa Tanzania ya viwanda  na kusema kuwa, kama taifa, linautolea macho mradi huo na kwamba serikali imedhamiria kuutekeleza.

Aliongeza kwamba, katika Serikali ya Awamu ya Tano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anayo imani kubwa  kuwa  miradi hiyo itaanza huku  serikali ikitegemea  kupeleka  maendeleo  kwa wananchi kupitia miradi husika.

 “Wizara yetu ndiyo inatoa leseni za madini na tayari tulishatoa leseni ya Makaa ya mawe mchuchuma kwa hiyo nimefika kuangalia changamoto ambazo ziko upande wa wizara yetu kuweza kuzitatua ili tutoke hapa. Miradi hii tumeisikia miaka mingi ni wakati sasa tunataka ianze.” alisisitiza Nyongo.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiangalia makaa ya katika mgodi wa Liganga alipoutembelea hivi karibuni. Naibu Waziri alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujua changamoto za utekelezaji wa mradi huo.

Aliongeza kuwa, ikiwa wizara ndiyo inatoa leseni za madini,  inaowajibu wa kujua yule aliyepewa leseni kama anaifanyia kazi na kuongeza, “Sisi tuliotoa leseni lazima tuangalie tuliyempa leseni amekwama wapi  lakini pia tujue  miradi hii inaanza lini? Makaa ya mawe na chuma vyote vinahitajika kwa taifa. Tunatambua makaa ya mawe ni madini ambayo yana tija kwa uchumi kwa nchi,” alisema Nyongo.

Akifafanua zaidi kuhusu miradi hiyo alisema kuwa, mradi wa Makaa ya Mawe unatarajiwa kuzalisha umeme ambao mbali ya kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umeme huo unatarajia kutumika katika kuzalisha madini ya Chuma Liganga.

 “Mpango ni Liganga kutumia megawati 250 kwa shughuli zake za kuzalisha chuma na megawati 350 zitauzwa Tanesco kuzalisha umeme,” aliongeza.

Akifafanua sababu za kuchelewa kwa miradi hiyo, alisema ni kutokana na changamoto za kimkataba ambazo bado ziko katika majadiliano katika ngazi za juu na kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni  kuwa ni pamoja na mikataba ya upunguzaji wa kodi.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza Meneja wa mgodi wa Kokoto wa Nyakamtwe Quary, uliopo mkoani Njombe alipoutembelea wakati wa ziara yake hivi karibuni.

Aliongeza kuwa, wizara ya madini ikiwa ni wizara ambayo inasimamia Sheria ya Madini, imelenga kuhakikisha kwamba miradi hiyo mikubwa inaanza ili hatimaye iweze kuwanufaisha watanzania na taifa.

Akielezea suala la fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, alianza kwa kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kwa kutenganisha suala la miradi hiyo na fidia  ambapo alisema kwamba taratibu za juu zikikamilika, wananchi watalipwa fidia  na hivyo kuwataka kuwa na subira na kuwa tayari kupisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali,  Mkuu wa Mkoa wa Njombe , Christopher Ole Sendeka alimweleza waziri umuhimu wa wizara ya madini kujielekeza  kwenye kupata taarifa halisi kuhusu tafiti zilizofanyika awali kuhusu  akiba iliyopo ya madini ya chuma  Liganga na Makaa ya Mawe mchuchuma.

Aidha, aliongeza kuwa, mbali na chuma na makaa ya mawe mkoa huo unayo madini mbalimbali ikiwemo dhahabu ambayo bado haijachimbwa kwa kiasi kikubwa.

Miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga, inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda Group Ltd, ya China.

Pia, akiwa mkoani humo, Naibu Waziri alitembelea mgodi wa Kokoko Kokoto wa Nyakamtwe Quary, ambapo alitoa changamoto kwa mmiliki wa mgodi huo kuongeza kasi ya uzalishaji na kuwa wabunifu kutumia fursa  za miradi mikubwa ya ujenzi  inayotekelezwa na serikali ikiwemo ya ujenzi wa reli ili kokoto hizo ziweze kutumika.

Read more

Naibu Waziri Nyongo Aamuru Kukamatwa Wamiliki Mgodi Wa Nyakavangala

Na Asteria Muhozya, Iringa

15/01/2019

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameamuru kukamatwa kwa Wamiliki wa mgodi wa Nyakavangala unaomilikiwa na  Thomas Masuka and Partners  kufuatia wamiliki hao kutofautiana juu ya taarifa  waliyoiwasilisha kwa Naibu Waziri kuhusu namna mgodi huo unavyoendeshwa ikiwemo ulipaji wa kodi na mrabaha wa serikali.

Aidha, Naibu waziri amewataka wamiliki hao kutoa maelezo ya kina kuhusu ni lini watalipa kodi zote wanazodaiwa na serikali baada ya kuonekana kuwa mgodi huo unadaiwa zaidi ya shilingi milioni 128 za mrabaha ambazo imedaiwa kuwa, wapo baadhi ya wamiliki ambao wamekuwa wakikusanya fedha hizo lakini zimekuwa hazilipwi.

Katika ziara yake mkoani humo, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na kujionea shughuli za uchimbaji katika migodi ya dhahabu ya Ulata na Nyakavangala, amebaini ukwepaji mkubwa wa kodi pamoja na mrabaha wa serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akimwonesha jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua migodi ya Nyakavangala.

Pia, amemtaka Afisa Madini kutoa maelekezo ya kina kuhusu suala zima la ulipwaji wa kodi na mrabaha wa serikali, huku akiagiza zoezi hilo pia limuhusishe Afisa Msimamizi wa madini aliyekuwepo katika kipindi ambacho fedha hizo hazikulipwa.

“Hatutaki ugomvi hapa kwenye migodi. Tunataka mgodi ufanye kazi. Dhahabu ziuzwe mahali panapoonekana. Hapa naona hesabu za viroba tu. Mnunuzi wa dhahabu hapa ni nani”, alihoji Naibu Waziri.

Wakati akizungumza na wachimbaji katika mkutano wa hadhara, amewataka wachimbaji hao kuchimba kwa kuzingatia usalama  huku akisisitiza suala la kufuata sheria na taratibu  huku akiwataka kutoa taarifa za  uhakika kwa wale wote wanaokikuka sheria ikiwemo watoroshaji wa madini huku akisisitiza  utoaji  taarifa hizo usiwe wa majungu.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akikagua moja ya mgodi katika mgodi wa Nyakavangala wakati wa ziara yake mgodini hapo. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.

Akitolea ufafanuzi suala la fedha za mrabaha, amesema fedha hizo hazipaswi kuelekezwa katika masuala mengine na wamiliki wa migodi ikiwemo kutumiwa katika huduma za jamii badala yake  zinapaswa kulipwa serikalini.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwataka wamiliki hao kukaa chini na kukubaliana namna ya kulipa kiasi cha fedha ambacho wanadaiwa na serikali huku akimtaka Afisa kutoka Halmashauri anayehusika na masuala ya usimamizi wa fedha kuhakikisha kwamba fedha ambazo mgodi huo ulipaswa kuzilipa kama mrabaha zinapatikana.

Mgodi huo wa Nyakavangala unamilikiwa na Thomas Masuka kwa ushirikiano na wawekezaji wengine wazawa wapatao 20. Wakati akiagiza kukamatwa kwao, wamiliki 8 kati ya 20 ndiyo walikuwa wamehudhuria kikao kati yake na wamiliki hao. Naibu Waziri Nyongo alitoa agizo hilo Januari 15 wakat akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani humo.

Read more

Waziri Biteko Akutana Na Kampuni Ya TANZAPLUS

Greyson Mwase; Dodoma

Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 16 Januari, 2019 amekutana na kampuni inayojishughulisha na uyeyushaji wa madini ya bati katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ya Tanzaplus katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo jijini Dodoma.  Kikao chake pia kilishirikisha Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Madini, Augustine Ollal, Mhandisi Migodi Mkuu kutoka Tume ya Madini, Conrad Mtui pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Madini.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akizungumza na watendaji wa kampuni inayojishughulisha na uyeyushaji wa madini ya bati katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ya Tanzaplus.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kampuni ya Tanzaplus Minerals kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya AIMGROUP kutambulisha teknolojia ya mfumo wa usimamizi wa uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa madini. Waziri Biteko aliitaka kampuni ya Tanzaplus kuendelea kufanya utafiti zaidi juu ya mfumo husika kwa kushirikisha wadau mbalimbali  kabla ya kuwasilisha pendekezo lake Serikalini.

Read more

Nyongo ataka wanaomiliki migodi kwa kuvamia wasimame mara moja

Na Asteria Muhozya, Iringa

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wanaomiliki migodi kwa kuvamia maeneo bila kuwa na leseni, wasimame mara moja.

Naibu Waziri Nyongo ametoa kauli hiyo katika mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayani Iringa, wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua shughuli za uchimbaji madini ikiwemo kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wadogo.

Aidha, kauli ya Naibu Waziri inafuatia mgogoro uliopo katika mgodi huo kati ya  mwenye leseni ya kumiliki mgodi huo Ibrahim Msigwa , wachimbaji wadogo wanaochimba katika eneo hilo na  Mansoor Almasi anayetajwa kuwa mmiliki mwingine na mnunuzi wa madini  ya dhahabu yanayochimbwa mgodini hapo ambaye kwa mujibu wa taratibu,  hana  vibali  vinavyomruhusu kufanya shughuli hizo.

Akilenga kutatua na kuumaliza mgogoro uliopo mgodini hapo, Naibu Waziri amemtaka Mansoor Almas, kufika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa ifikapo Januari 15, na endapo atakiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiteta jambo na Maafisa alioongozana nao katika ziara ya kukagua na kutatua mgogoro katika mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayani Iringa.

“Sisi kama serikali ambao ndiyo tunatoa vibali tunamtambua bwana Msigwa kuwa ndiye mmiliki halali. Nataka kuonana na huyu Mansour na yoyote anayedharau serikali tutakula nae sahani moja,” alisisitiza Naibu Waziri. 

Naibu Waziri alisema lengo la kutaka Mansour kufika wilayani hapo ni kutaka kusikia kutoka pande zote ili mgogoro huo uweze kutatuliwa na kufika mwisho jambo ambalo litawezesha shughuli za uchimbaji katika eneo husika kuendelea vizuri ili pande zote yaani serikali na wachimbaji wanufaike.

Akifafanua kuhusu suala la shughuli za uchimbaji, Naibu Waziri amesisitiza kuwa, ili kuwa mchimbaji halali ni lazima kuwa na kibali kutoka serikalini na kuongeza kwamba, ni vigumu kuomba kwenye leseni ya mtu mwingine.

Pia, amewataka wachimbaji wadogo kutoshirikiana na wale wote wanaopindisha utekelezaji wa sheria na taratibu katika shughuli za uchimbaji madini na badala yake washirikiane na wale wenye vibali vya umiliki kutoka serikalini.

Sehemu ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Mlata, Kijiji cha Mrata, Kata ya Uwasa Wilaya ya Iringa wakifuatilia mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. (hayupo pichani).

Pia, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wale wote wasiokuwa na uwezo wa kuchimba kuingia mikataba na wachimbaji wengine wenye uwezo ili kuwezesha lengo la kumiliki leseni kutimia kwa kuhakikisha kwamba zinafanyiwa kazi. “unaweza kuingia mkataba na mchimbaji  wengine wakiwemo wa kati

“Nataka muelewe kwamba, mnaochimba mnachimba kwa niaba ya watanzania kwa sababu watanzania ambao siyo wachimbaji. Hawa wanafaidika kutokana na kodi na mrabaha unaolipwa kutokana na shughuli zenu, kwa kuwa fedha hizo zinatumika katika kutoa huduma nyingine,” alisema Nyongo.

Awali, wachimbaji hao waliwasilisha kero kwa Naibu Waziri kuhusu mgogoro wa umiliki wa mgodi huo umesababisha shughuli za uchimbaji mgodini hapo kuwa mgumu suala ambalo linasababisha ugumu wa kupata kipato cha kujikimu na kuendesha familia zao.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao chake na watendaji wa Mkoa wa Iringa kabla ya kuanza ziara ya kukagua shughuli wa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Ulata.

Wachimbaji wao walimshukuru Naibu Waziri kwa kufika kwake mgodini hapo ambapo walipata fursa ya kueleza kero ikiwemo suala la bei elekezi ya madini hayo ambalo walimlalamikia kuwa, wamekuwa wakiwauzia wanunuzi wa madini hayo akiwemo Mansoor Almasi na Ibrahim Msigwa kwa kiasi cha shilingi 45,000 kwa gramu moja jambo ambalo Naibu Waziri ameeleza kuwa, atakapoonana na wahusika hao atawaeleza kuhusu suala hilo.

Akitoa utetezi wake kwa Naibu Waziri kuhusu kero zilizowasilishwa dhidi yake na wachimbaji hao, Msigwa amesema mazingira mabaya mgodini hapo yaliyowasilishwa na wachimbaji yanatokana na kuwepo kwa kesi mahakamani jambo ambalo linamfanya ashindwe kuendelea na shughuli za uchimbaji kama inavyompasa.

 Wakati huo, huo,  katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Iringa, Katibu Tawala wa Mkoa huo Happines Seneda, alimweleza Naibu Waziri kuhusu umuhimu wa kuwa na Afisa Madini wa Mkoa huo badala ya kutegemea AFisa Madini wa Mkoa wa Njombe jambo ambalo ameeleza kwamba, uwepo wake mkoani humo utaongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa shughuli za madini.

Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri Stanslaus Nyongo alimweleza Katibu Tawala huyo kuwa, Wizara imelenga kuhakikisha kwamba kila Mkoa unakuwa na Afisa Madini baada ya kuondolewa kwa Makamishna wa Madini wa Kanda kufuatia Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017.

Naibu Waziri Nyongo alitembelea mgodi huo Januari 14, 2019.

Read more

Wachimbaji madini Suguta wapata leseni

Watoa pongezi kwa Mwenyekiti Tume ya Madini

Na Greyson Mwase, Dodoma

Januari 16, 2019

Kikundi cha wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu” kimepongeza Tume ya Madini kwa kutatua mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu pamoja na kuwapatia leseni.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 16 Januari, 2019 katika makabidhiano ya leseni ya uchimbaji wa madini hayo katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma zilizopo jijini Dodoma.

Kutatuliwa kwa mgogoro kati ya kikundi hicho na wananchi wa kijiji cha Suguta ni matokeo ya ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliyoifanya mapema Septemba 05, 2018 katika machimbo hayo na kukuta kikundi hicho kikiendesha shughuli za uchimbaji wa madini pasipo kusajiliwa na kutokuwa na leseni ya uchimbaji wa madini.

Mara baada ya kufanya ziara katika eneo husika Profesa Kikula alielekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa  Dodoma, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius John Ndejembi kuhakikisha kikundi cha wachimbaji hao kinasajiliwa na kupatiwa leseni ndani ya muda mfupi.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) akimkabidhi leseni ya madini Mwenyekiti wa Kikundi cha wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu”, Elisha Cheti (kushoto)

Aidha, Profesa Kikula alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto kuhakikisha mgogoro uliokuwepo kati ya kikundi hicho na wananchi wa kijiji cha Suguta unamalizika.

Akitoa shukrani hizo kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa kikundi cha “Hapa Kazi Tu” Elisha Cheti alisema kuwa ziara ya Profesa Kikula ilipelekea kuongezeka kwa kasi ya usajili wa kikundi na hatimaye wakafanikiwa kuomba leseni ya kuchimba madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma.

Alisema mara baada ya kupata leseni pamoja na barua ya utambulisho wanatarajia kuanza shughuli za uchimbaji madini na kulipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.

Naye  Mwenyekiti wa DOREMA, Kulwa Mkalimoto mbali na kuipongeza na kuishukuru Tume ya Madini kwa utoaji wa leseni amekitaka kikundi kilichopewa leseni kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufuata sheria na kanuni za madini huku kikihakikisha hakuna uharibifu wowote wa mazingira.

Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano akizungumza wakati wa makabidhiano hayo alifafanua kuwa, maombi ya leseni ya uchimbaji wa madini ya kikundi husika yalipitishwa kupitia kikao cha Kamati ya Ufundi ya Tume kilichokaa tarehe 22 Novemba, 2018.

Mwano alitoa wito kwa wachimbaji wadogo wasio rasmi kuunda vikundi, kusajili na kuomba leseni na kusisitiza kuwa ofisi yake itahakikisha leseni za madini zinatolewa kwa kasi ili waweze kuchimba pasipo kusumbuliwa huku wakilipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.

“Sisi kama Tume, tunaamini wachimbaji wadogo wana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa sekta ya madini; tunaunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli za kuhakikisha watanzania wote wananufaika na rasilimali za madini,” alisisitiza Mwano.

Read more

Biteko akutana na wawekezaji mradi wa uchimbaji wa uranium

Na Nuru Mwasampeta, Dodoma

Januari 16, 2019

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka  kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini  ya uranium katika mto Mkuju ulioko mkoani Lindi ya Uranium One  kutokusita kuwasiliana naye pindi wanapokutana na changamoto katika utekelezaji wa  mradi wao.

Aliyasema hayo tarehe 15 Januari, 2019 katika kikao chake na watendaji wa kampuni hiyo kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma.

Aidha, Biteko alisema kuwa maombi yote ya leseni kubwa za uchimbaji wa madini zinawasilishwa katika baraza la Mawaziri ili kuweza kuridhiwa baada ya wawekezaji kuonesha nia na kuwasilisha maombi ya leseni hizo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko akimsikiliza Makamu wa Rais wa kampuni ya Uranium One Holdings N.V, Vladimir Hlavinka akielezea nia yao ya kutaka kuwekeza katika sekta ya madini nchini wakisubiri uwekezaji wao katika masuala ya uranium uliositishwa kwa muda.

Biteko alikiri kuwa anao uelewa wa kile kinachoendelea katika uwekezaji huo kutokana na ushirikishwaji alioupata kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki kupitia vikao mbalimbali alivyoshiriki.

Akizungumzia lengo la ujio wao katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uranium One, Frederick Kibodya alisema ni kuelezea maendeleo waliyofikia katika uwekezaji huo pamoja na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Madini.

Alisema, uteuzi huo umelenga katika kukuza sekta ya madini ikiwa ni pamoja na mradi wa uchimbaji wa madini ya uranium, “Tunaimani kubwa kwako na tunamshukuru Mungu kwa kukupa nafasi hii” alisema Kibodya.

Akizungumzia uwekezaji uliofanyika mpaka sasa katika mradi huo alisema ni kiasi cha dola za kimarekani Milioni mia mbili ($200mil) kutoka mradi ulipoanza mwaka 2009.  

Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wawekezaji kutoka kampuni ya Uranium One Holdings N.V waliofika kuzungumzia nia yao ya kuwekeza katika maeneo mengine ya madini nchini

Akizungumzia manufaa ya mradi huo Kibodya alisema ni pamoja na kusaidia katika kukuza teknolojia nchini. Alisema madini hayo yakichimbwa yanatumika katika kuzalisha umeme ambayo ni teknolijia mpya nchini.

Mradi utasaidia katika kuongeza ajira nchini. Aliendelea kufafanua kuwa kwa kipindi cha ujenzi wa mradi wanatarajia kuajiri watanzania 1600 kwa kipindi cha miezi kumi na nane.

Aidha, alibainisha kuwa kutakuwepo na uzalishaji wa ajila zisiso rasmi kiasi cha watu 4500 wakati wa ujenzi na 2300 pindi uzalishaji utakapoanza.

Alisema, mradi utasaidia katika kuhamisha utaalamu kutoka kwa wawekezaji kwenda kwa wazawa na mradi umelenga katika kutoa elimu ya ajira na utaalamu kwa wazawa.

Pia Kibodya alisema, mradi unatarajia kuliingizia taifa pato la kiasi cha dola za kimarekani milioni 220 kama kodi kwa mwaka, kiasi ambacho kitakuwa kikibadilika kadri uzalishaji unavyoongezeka.

Mradi wa uchimbaji madini ya uranium katika mto Mkuju unafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Mbia wa kampuni ya Mantra anayejulikana kama Rosatom.

Read more

Naibu Waziri Aagiza Wanunuzi Haramu Wa Dhahabu Ulata Kukamatwa

Kufuatia kukaidi Wito wa kuonana na Naibu Waziri wa Madini  Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela    kutokana na kufanya ununuzi haramu wa madini ya dhahabu ikiwemo kufadhili uchimbaji haramu, Naibu Waziri Nyongo amevitaka vyombo vya  Ulinzi na Usalama mkoani Iringa kuwakamata Mansoor  Almasi na Jacob Mwapinga iwapo watashindwa kuripoti wenyewe katika Mamlaka zinazohusika.

Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo la kukamatwa wahusika hao baada ya kukiuka agizo la kuonana na viongozi hao kwa hiari ambapo walielekezwa kuonana na Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa Januari 15, 2019.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza mmoja wa wawekezaji katika eneo la Nyakavangala Kazi Kuboma alipofika katika eneo lake ili kuona namna anavyoendesha shughuli zake uchenjuaji madini. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela na Maafisa Madini na Maafisa wa Wilaya.

Pia, kabla ya wito wa Naibu Waziri, awali, wahusika hao walitakiwa kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Iringa wakiwemo Maafisa Madini kwa ajili ya kuupatia suluhisho mgogoro huo katika mgodi wa dhahabu wa Ulata, kijiji cha Ulata wilaya ya Iringa unaomilikiwa na Ibrahimu Msigwa.

Naibu Waziri Nyongo alibaini kuwa Mansoor na Mwapinga wanafanya ununuzi wa madini kinyume cha Sheria ikiwemo kufadhili shughuli za uchimbaji katika mgodi ambao siyo wamiliki wake.

Pia, Naibu Waziri ameelekeza baada ya wahusika hao kukamatwa wanatakiwa kutoa maelezo kueleza ni lini watalipa kodi wanazodaiwa na serikali baada ya kufanya shughuli hizo bila kulipa kodi.

Akizungumza  katika mkutano wa hadhara na wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo aliwaeleza kuwa, Serikali inamtambua Ibrahimu Msigwa kama mmiliki halali baada ya kuwa na vibali vya kumiliki leseni ya mgodi huo na hivyo kutoa wito wa kuonana na pande zote ili kuhakikisha  kuwa anatoa suluhisho la mgogoro uliopo baina ya Msigwa, Mansoor, Mwapinga na wachimbaji.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akimweleza jambo mmoja wa wachimbaji wakati akikagua mazingira ya uchimbaji madini katika mgodi wa Nyakavangala. Wanaomfuata ni baadhi ya wachimbaji wadogo wanaochimba katika mgodi huo.

Akihitimisha ziara yake mkoani Iringa Januari 15, Naibu Waziri Nyongo amesema kuwa, amebaini ukwepaji mkubwa wa kodi katika migodi ya Ulata na Nyakavangala.

Amesema wamiliki wa leseni wanaotumia mrabaha kwa ajili ya kufanya masuala mengine ya kijamii wanakiuka taratibu na kueleza kuwa, fedha za kufanyia shughuli za maendeleo zinapaswa kutoka katika fedha za Uwajibikaji kwa jamii ambazo halmashauri zinapanga kupitia Baraza la Madiwani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema wahisika  Mwapinga na Almasi wana kiburi na kwamba waliitwa kwa ajili ya kuongea ili ku[ata fursa ya kujieleza na a kueleza ni lini watalipa mrabaha  lakini wamekaidi hivyo kinachofuatia ni wahusika kukamatwa.

Naibu Waziri Nyongo alifanya ziaea katka mgodi wa Ulata Janauri 14 akilenga kukagua shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo ikiwemo kutatua mgogoro uliokuwep katika mgodi huo baina ya mmiliki halali Ibrahimu Msingwa, wanunuzi haramu wa madini hayo Mansoor Almasi na Jacob Mwapinga.

Read more