Archives for News & Events

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Azindua Soko la Madini Chunya

Na Greyson Mwase, Chunya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amezindua Soko la Madini Chunya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka Wilaya ya Chunya kuhakikisha imekamilisha na kuzindua soko la madini ndani ya kipindi cha siku saba. Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 27 Aprili, 2019 wilayani Chunya katika mkutano wake na wachimbaji na wachenjuaji wa madini.

Uzinduzi huo ulishirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi,  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Ali Ali.

Wengine walioshiriki katika uzinduzi huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, wawakilishi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari.

Watendaji kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Idara nyingine za Serikali wakifuatilia hotuba ya uzinduzi wa Soko la Madini Chunya iliyokuwa inatolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila. (hayupo pichani).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Profesa Msanjila alisema kuwa, tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Sekta ya Madini inakua, inanufaisha watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.

Akielezea mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi  wa rasilimali za madini, Profesa Msanjila alisema kuwa,  ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufahika na rasilimali za madini, Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi  Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili Namba 5 ya Mwaka 2017; Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Namba 6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123.

Aliendelea kueleza kuwa Serikali pia imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo na kufafanua kuwa tozo hizo kuwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo.

Alisema kuwa, kuwekwa kwa mazingira mazuri ya kibiashara kwenye sekta ya madini pamoja na kufuta kodi na tozo mbalimbali zinazofikia asilimia 23 kutaondoa utoroshwaji wa madini na kusaidia wachimbaji wadogo kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini.

Alieleza manufaa mengine kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa mapato ya nchi. Katika hatua nyingine, Profesa Msanjila aliwataka  wachimbaji wote wadogo na wafanyabiashara wa madini  kuendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali  za Serikali katika kutekeleza majukumu  yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali  inayotolewa na Serikali.

Akielezea manufaa ya soko jipya la madini Chunya, Profesa Msanjila alisema soko litaziba mianya ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi na hivyo kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya uzinduzi kabla ya kuzindua Soko la Madini Chunya.

Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya kutawezesha na kurahisisha biashara nzima ya madini na kuwa kiungo muhimu cha kuwakutanisha wachimbaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuuza na kununua madini. Profesa Msanjila aliendelea kufafanua manufaa mengine ya soko kuwa ni pamoja na kuwa suluhisho la tatizo la kupunjwa na kudhulumiwa na kuondoa  vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa  vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo.

“Soko hili litaondoa  uwezekano wa wanunuzi  wa madini kuibiwa na wajanja wachache wanaojifanya  kuwa na madini wakati hawana, nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko kikamilifu ili kuepuka udanganyifu na matapeli tu” alisema Profesa Msanjila.

Katika hatua nyingine Profesa Msanjila aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Chunya, wafanyabiashara wa madini kwa kuhakikisha Soko la Madini Chunya limezinduliwa ndani ya muda uliopangwa.

Wakati huo huo akizungumzia hali ya uanzishwaji wa masoko ya madini nchini, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa, hadi kufikia sasa masoko matano ya madini yameshafunguliwa katika mikoa ya Geita, Singida, Kahama, Arusha – Namanga na Chunya.

Aliongeza kuwa masoko mengine ya madini yanatarajiwa kufunguliwa kabla ya tarehe 05 Mei, 2019 ikiwa ni pamoja na Soko la Madini ya Dhahabu na Vito vya Thamani Ruvuma, Soko la Madini Shinyanga, Soko la Madini Dodoma na Soko la Madini Mbeya.

Profesa Kikula alitaja masoko mengine ambayo yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni kuwa ni pamoja na Soko la Madini ya Bati (tin) na Soko la Madini ya Dhahabu Handeni. Alisisitiza kuwa mikoa mingine ipo katika  hatua za mwisho kukamilisha vigezo mbalimbali vikiwemo vya kiusalama na miundombinu.

Read more

Tunataka Kurahisisha Mazingira Biashara Ya Madini – Biteko

Naibu Waziri Nyongo ataka Soko la Madini Arusha kuanzishwa haraka

Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Serikali kupitia Wizara yake inalenga kurahisisha Mazingira ya Biashara ya Madini ikiwemo kuwalea wachimbaji na kuwataka wafanyabiashara na wachimbaji kuhakikisha wanajisimamia wenyewe kwa manufaa yao na Taifa.

Waziri Biteko ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Sam Mollel ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 10, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu biashara ya madini nchini.

Amekitaka chama hicho kuendelea kushirikiana na wizara kwa lengo la kusukuma mbele Sekta ya Madini ikiwemo kuhakikisha biashara ya madini inafanyika katika mazingira yenye kuzinufaisha pande zote na kuwasisitiza viongozi hao kuhakikisha wanachama wao wanafuata taratibu wanapofanya biashara ya madini.

Awali, kabla ya kujibu hoja zilizowasilishwa na chama hicho, Waziri Biteko amekipongeza chama hicho kwa kuwa kimekuwa kikitoa njia mbadala pindi kinapowasilisha changamoto na kero zake badala ya kuishia kulalamika na kuongeza, “wizara inaona fahari kwa hilo na tunayachukulia kwa umuhimu maoni yenu,”.

Akizungumzia suala la kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio ambayo imeondolewa kwenye uchimbaji mdogo, Waziri Biteko amekitaka Chama hicho kutoa nafasi kwa serikali kufuatilia suala hilo. Waziri Biteko ameleeza hilo kufuatia hoja iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel ambaye ameeleza kuwa, katika mkoa wa Arusha, kodi hiyo bado inatozwa licha ya serikali kuiondoa.

Waziri wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na Viongozi wa (TAMIDA) pamoja na Viongozi Waandamizi wa Wizara baada ya kikao.

Aidha, Waziri Biteko ametolea ufafanuzi wa changamoto kadhaa zilizowasilishwa na Mwenyekiti Sam Mollel kwa niaba ya chama hicho ikiwemo. Kuhusu bei elekezi, Waziri Biteko amesema wizara itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha suala hilo linakuwa shirikishi. Waziri Biteko amesema hilo baada ya TAMIDA kutoa pongezi kwa serikali kwa kutoa nafasi kwa wadau kukaa pamoja na serikali kujadili suala la bei elekezi ambapo Mwenyekiti huyo amemweleza Waziri Biteko kuwa, katika hilo, serikali na wadau wameanza vizuri.

Akitolea ufafanuzi kuhusu suala la kurejesha maonesho ya madini jijini Arusha, Waziri Biteko amesema suala la maonesho ya madini kufanyika arusha inawezekana lakini si kwa madini ya Tanzanite, na kuongeza kuwa, serikali imedhamiria kufanya shughuli zote zinazohusu madini hayo ndani ya ukuta unaozunguka machimbo ya mirerani lakini pia ikilenga kuubadilisha mji wa mirerani ufanane na madini hayo.

Aidha, Waziri Biteko amezungumzia suala la kuongeza wataalam wa kuthamini madini ya Tanzanite Mirerani na kueleza kuwa, kutokana na unyeti na umuhimu wa suala hilo, tayari serikali imeanza kulifanyia kazi ili kuhakikisha inaongeza idadi ya wataalam kuwezesha shughuli za uthamini Mirerani, kufanyika kwa wakati. Ufafanuzi huo umetolewa baada ya Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel kuwasilisha changamoto ya kuwepo na upungufu wa wataalam hao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza katika kikao hicho, ametaka kuanzishwa haraka kwa soko la Madini jijini Arusha na kueleza kuwa, kwa upande wa wizara itahakikisha inashirikiana na serikali ya mkoa kuhakikisha soko hilo linaanzishwa haraka. Naibu Waziri Nyongo amesema hayo akijibu hoja ya Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel ambaye ameleeza katika kikao hicho kuwa, Chama hicho kinaunga mkono Serikali kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini na kuitaka serikali ione umuhimu wa kuanzisha soko La madini la madini mkoani arusha kuwezesha biashara ya madini ya vito kufanyika kwa urahisi.

Kuhusu vibali vya Wataalam wa masuala ya ukataji na unga’rishaji wa madini kutoka nje ya nchi, Naibu Waziri Nyongo amesema kuwa, ni kweli kwamba serikali inawahitaji wataalam hao kwa kuwa pia watawezesha kutoa ujuzi huo kwa wataalam wa ndani ili kuhamasisha viwanda vya ukataji madini na kuongeza, “serikali inaangalia namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika kwa sababu pia tunataka watu wetu wanufaike na utaalam huo”.

Pia, ameongeza kuwa, kutokana na kulichukulia suala la uongezaji thamani madini kwa umuhimu, inakitegemea kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa ajili ya kuzalisha wataalam na kukitaka chama hicho kusaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika kituo hicho kwa kuwa hivi sasa idadi bado ni ndogo.

Kikao hicho cha Waziri na TAMIDA ni cha kwanza tangu kuteuliwa kwa Waziri wa Madini Doto Biteko kuiongoza wizara husika. Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Viongozi Waandamizi kutoka wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Read more

Wananchi watakiwa kumpisha mwekezaji kuchimba dhahabu

Na Greyson Mwase, Shinyanga

Aprili 03, 2019

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga kumpisha mwekezaji  ambaye ni  mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu wa kampuni ya  Hanan Afro Asia Geo Engineering (T) Limited kutoka China  kuendelea na maandalizi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu, kwa kuwa ndiye aliyewekeza katika kijiji husika kwa kufuata sheria na kanuni zake.

Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03 Aprili, 2019 katika mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Shinyanga yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Kamando, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa, wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

Kutoka kushoto mbele, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakinukuu kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.

Alisema kuwa, kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na mwekezaji kutoka nchini China ambaye ni  kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited ambapo malalamiko yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kahama Machi 10, 2018 ambapo alielezwa kuhusu unyanyasaji  uliofanywa wakati wa zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupisha uanzishwaji wa mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu.

Aliendelea kusema kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli Machi 11, 2018 aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitembelea eneo la Mwakitolyo linalolalamikiwa kwa lengo la kufanya mkutano na kusikiliza malalamiko ya wananchi ambapo baada ya kusikiliza malalamiko hayo aliahidi kwenda kufanyia kazi malalamiko yao na kuwapa mrejesho.

Aliendelea kueleza kuwa, iliundwa timu maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kulingana na hadidu rejea iliyokuwa imepewa ambayo iliitaka timu kukutana na viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya, kuainisha majina ya wananchi waliolipwa na ambao hawajalipwa fidia, vigezo vilivyotumika wakati wa uthaminishaji na ulipaji wa fidia pamoja na mapendekezo mbalimbali.

Nyongo aliendelea kufafanua kuwa, mara baada ya timu kumaliza kazi yake, ilibainika kuwa mwekezaji alilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.63 kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo husika hivyo zoezi kukamilika kwa asilimia 99.6.

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo (hawapo pichani)

Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi takribani 375 kulipwa fidia bado ilionekana kuwa wananchi wengi waliolipwa fidia sio wanakijiji wa Mwakitolyo na kuongeza kuwa wananchi 40 tu ndio walioonekana wamiliki halali wa mashamba pamoja na makazi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuharakisha upatikanaji wa maeneo mapya kwa ajili ya wanananchi 40 ambao ni wamiliki halali wa makazi na mashamba katika kijiji cha Mwakitolyo ili mwekezaji aweze kuanza shughuli za uchimbaji mara moja.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited kuhakikisha anadumisha mahusiano na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na kumtaka kuhakikisha anashiriki katika uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, barabara kama Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake inavyofafanua.

Wakati huo huo Nyongo aliwataka wananchi kumpa ushirikiano mwekezaji ili kufaidi matunda ya uwekezaji kwenye kijiji chao ikiwa ni pamoja na ajira kwa wazawa, utoaji wa huduma za vyakula, biashara, huduma za jamii hivyo kupaisha uchumi wa kijiji hicho.

Aliendelea kusema kuwa, madini ni mali ya watanzania wote, hivyo baada ya uwekezaji kuanza kampuni hiyo italipa kodi mbalimbali kwenye halmashauri na Serikali kuu hivyo kuboresha sekta nyingine kama vile miundombinu, afya, elimu n.k.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akizungumza katika mkutano huo mbali na kumpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutatua mgogoro huo, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii huku wakilinda amani ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited, Zhang Jiangho mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kutatua mgogoro huo  uliodumu kwa muda mrefu, aliahidi kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kwa kuboresha  huduma za jamii na kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

Read more

Waziri wa Madini Uganda afurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini Nchini

Na Greyson Mwase, Geita

Aprili 02, 2019

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris amesema kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania na kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma wataalam wake pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Lokeris aliyasema hayo tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini hususan katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.

Akiwa ameongozana na  ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo aliwasili mkoani Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (wa pili kulia) akifafanua jambo kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo mara baada ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara kwenye mgodi huo. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.

Ziara hiyo pia ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.

Akielezea hali iliyopelekea nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya utafiti katika nchi za Aftika Mashariki, walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi wa sheria na kanuni za madini hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo hususan wachimbaji wadogo wa madini.

Aliendelea kusema kuwa, Sekta ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema kuja Tanzania kwa ajili ya kujifunza na kwenda kuimarisha Sekta ya Madini ili baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.

Akielezea mikakati ya matumizi ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania, Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini wa Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Aliendelea kueleza kuwa, nia ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje ya nchi na kujipatia mapato makubwa.

Mtaalam kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Busolwa uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita, Felix Adolf Ishebabi (katikati) akielezea shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinavyofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris, Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo.

“Tumefurahishwa na usimamizi mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia sheria na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.

 Naye Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini nchini alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji wa sheria mpya ya madini pamoja na kanuni zake inayotambua madini kama mali ya watanzania na kusisitiza kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wanufaika kwa kiasi kikubwa.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima hali iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.

Naye mmiliki wa mgodi wa dhahabu wa Blue Reef uliopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza na ujumbe huo uliofanya ziara kwenye mgodi wake akielezea mchango wa mgodi wake katika jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka 1991 mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi 160 na vibarua takribani 200.

Afisa Migodi Mkazi wa Mkoa wa Geita, Ernest Maganga (kulia) akielezea namna biashara ya madini inavyofanyika kwenye Soko la Madini la Geita kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (kushoto) na Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo (katikati) pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi umekuwa ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali kama vile Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Chuo Cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya Madini na mashirika mengine ya kimataifa.

Aidha, aliongeza kuwa mgodi wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Akielezea mikakati ya mgodi wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini alisema mgodi wake unatarajia kufanya utafiti zaidi ili kugundua madini zaidi na kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na kutoka kwenye uchimbaji wa kati hadi mkubwa.

Read more

Waziri Biteko Awasimamisha Kazi Maafisa Madini Ofisi Ya Madini Chunya

Na Tito Mselem, Chunya

01/04/2019

Waziri wa Madini Doto Biteko amewasimamisha kazi Maafisa Madini wote wa Ofisi ya Madini Chunya Mkoani Mbeya na kuteua Wajiolojia watakaokaimu nafasi hizo wakati wizara ikitafuta Maafisa wengine waaminifu watakaofanya kazi hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kugundua wizi mkubwa wa madini ya dhahabu unaofanywa na maafisa hao wakishilikiana na wamiliki wa kampuni ya uchenjuaji wa dhahabu.

Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo wadogo pamoja na wamiliki wa makampuni ya uchenjuaji wa dhahabu Waziri Biteko, amesema udanganyifu unaofanywa na Maafisa hao wa Madini pamoja wenye  kampuni hizo za uchenjuaji ni mkubwa na  hahuitaji msamaha hata kidogo.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana katika sekta hii ya Madini ninawapenda sana wachimbaji ila nasikitika sana kwa wachimbaji na wenye makampuni ya uchenjuaji kutokuwa waaminifu,” amesisitiza Waziri Biteko

Ameongeza kuwa, Maafisa wa madini hao ndiyo wanaotoa mianya ya wizi wa dhahabu unaofanyika kwenye kampuni zaa uchenjuaji wa dhahabu wilayani humo.

Aidha, katika ziara hiyo Biteko ameifunga kampuni ya   Ntorah Gold Company Ltd inayohusika na uchenjuaji wa dhahabu wilayani humo baada ya kutoa taarifa za udanganyifu kwa serikali.

Pia, Waziri Biteko ameongeza kwamba, Wilaya ya Chunya ndiyo sehemu pekee Tanzania inayoongoza kwa wizi wa dhahabu na kutoa taarifa za uongo za kampuni za uchenjuaji wa dhahabu ikifuatiwa na wilaya ya Kahama iliyopo Mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjla, amesema serikali imeondoa kodi zote kwa wachimbaji wadogo zilizokuwa zikilalamikiwa na wachimbaji pamoja na kampuni za uchenjuaji wa dhahabu lakini bado wizi unafanyika tena kwa kiwango kikubwa.  

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila amikiri kwamba hana elimu ya madini hivyo imekuwa vigumu kwake kudhibiti wizi huo   lakini anaamini wizi na udanganyifu upo tena kwa kiwango kikubwa.

“kiukweli sina elimu ya madini hasa kwenye upande wa uchenjuaji wa dhahabu, naamini kuna wizi mkubwa wa madini haya ya dhahabu na taarifa zisizo na ukweli”amesema  Chalamila.

Read more

Waziri Wa Madini Uganda, Atembelea Tanzania

Greyson Mwase na Remija Salvatory, Mwanza

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris pamoja na ujumbe wake wameanza ziara nchini Tanzania leo tarehe 01 Aprili, 2019 yenye lengo la kujifunza namna sekta ya madini nchini Tanzania inavyoendeshwa. Waziri Lokeris ameongozana na maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo. Waziri wa Madini Nchini Uganda pamoja na ujumbe wake walipokelewa na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo kupitia mahojiano maalum aliyoyafanya na vyombo vya habari, mara baada ya kupokelewa na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo, Waziri Lokeris alisema kuwa lengo la ziara yake ni kujifunza sheria na kanuni za madini nchini Tanzania zinavyosimamiwa vyema pamoja na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji wa madini nchini Tanzania kwa vitendo kupitia wawekezaji waliowekeza nchini pamoja na wachimbaji wa wadogo wa madini.

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (wa pili kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

“Tulifanya utafiti na kubaini Tanzania ni  nchi yenye utajiri mkubwa wa madini na uzoefu mkubwa kwenye uchimbaji wa madini na tumeona wachimbaji wadogo wakisaidiwa sana na Serikali ya Tanzania,” Alisema Lokeris.

Aliongeza kuwa,  kati ya maeneo wanayotarajia kujifunza ni pamoja na ushirikishwaji wa wazawa kwenye  shughuli za uchimbaji wa madini (local content) utoaji wa huduma kwa jamii inayozunguka shughuli za uchimbaji wa madini (corporate social responsibility), usimamizi wa sheria ya madini pamoja na kanuni zake.

Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo, akielezea mafanikio ya nchi ya Tanzania kwenye usimamizi wa sekta ya madini kwa ujumbe wa Uganda.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Uganda umekuwa ni wa muda mrefu na kusisitiza kuwa Serikali ya Uganda ipo tayari kujifunza na kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi wa sekta ya madini.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali ya Tanzania inapenda kuona wananchi wake hususan waishio vijijini wananufaika na sekta ya madini kupitia uboreshwaji wa huduma za jamii kama vile elimu huduma za afya, na ili kuhakikisha wananchi wake wananufaika, Serikali imeamua kutuma wataalam wake Tanzania kujifunza kutokana na hatua kubwa iliyopigwa na nchi ya Tanzania kwenye usimamizi wa sekta ya madini.

Akielezea changamoto kwenye usimamizi wa sekta ya madini kwa nchi ya Uganda, Waziri Lokeris alieleza kuwa ni pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kutosha kwenye uongezaji thamani wa madini pamoja na utoroshwaji wa madini unaofanywa na wachimbaji wadogo.

Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (waliosimama katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka nchini Uganda na Tanzania.

Wakati huohuo Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo alisema kuwa nchi ya Tanzania ipo tayari kutoa uzoefu wake kwenye usimamizi wa sekta ya madini kwa nchi ya Uganda kupitia wataalam wake.

Alisema katika ziara ya ujumbe huo, mbali na nchi ya Tanzania kutoa uzoefu wake kwenye usimamizi wa sekta ya madini nchini, wanatarajia kuupeleka ujumbe huo kwenye soko la madini mkoani Geita lililozinduliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa pamoja na baadhi ya mitambo ya kuchenjulia dhahabu.

Akielezea mikakati ya Serikali ya Tanzania kwenye usimamizi wa sekta ya madini, Naibu Waziri Nyongo alieleza kuwa ni pamoja na uboreshaji wa sheria ya madini pamoja na kanuni zake ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini.

Alieleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini katika kila mkoa ili kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini.

Read more

Wizara itaendelea kuanzisha masoko ya Madini – Biteko

Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kusimamia Uanzishwaji wa Masoko ya Madini katika maeneo mbalimbali nchini huku ikiendelea kufanya marekebisho ya Kanuni za Uanzishwaji wa masoko hayo.

Waziri wa Madini Doto Biteko ameysema hayo Machi 31, 2019 wakati akifunga Semina ya siku mbili iliyoandaliwa na wizara kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati zenye uhusiano na Sekta ya Madini.

Semina hiyo ililenga kutoa elimu na kujenga uelewa wa pamoja kwa wabunge hao kuhusu sekta ya madini ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.

Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila (Kulia) wakati wa semina ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini, mafanikio na changamoto ya Shirika la Madini la Taifa STAMICO), elimu kuhusu majanga ya asili (hasa matetemeko ya ardhi), ukaguzi migodini, biashara ya madini na shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Uwazi na uwajibikaji katika Rasiimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia.

Waziri Biteko aliongeza kuwa, Wizara itaendelea kuwaelea wadau wa madini huku akiwataka kubadilika na kutenda matendo yenye manufaa kwa pande mbili na kuwaomba wabunge hao kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa wadau wa madini ili waweze kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati nyingine wakifuatilia uwasilishaji wa mada uliotolewa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake.

Pia, alisema serikali itaendelea kufanya kaguzi migodini kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji wanachimba kwa usalama na kueleza kuwa, wizara imeomba kibali cha kuongeza maeneo mengine ya ukaguzi wa madini na kusema, “tumepanga kuongeza vituo vingine 85”.

Aidha, alizungumzia maeneo yenye wizi wa dhahabu katika maeneo ya kuchanjua madini hayo na kuyataja kuwa ni Kahama na Chunya na kuwataka wahusika kuzingatia sheria na

Akizungumzia suala la kupunguza zaidi kodi kwa uchimbaji mdogo wa madini, alisema serikali haitapunguza tena kodi hizo kwa sasa mpaka hapo itakapoona manufaa yake.

Baadhi ya Watendaji na Wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake wakifatilia uwasilishwaji mada uliotolewa na Wataalam wa Wizara ya Madini na taasisi zake.

Ikumbukwe kuwa, baada ya mkutano wa Kisekta uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa madini baada ya wadau hao kuwasilisha kero zao kubwa ikiwa kodi, serikali ilifanya mabadiliko na kuondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo wa madini kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT (18%) na kodi ya zuio (withholding tax).

Mbali na wajumbe wa kamati, wengine walioshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Watendaji na Wataalam kutoka wizara na taasisi zake.

Read more

Naibu Waziri Nyongo Afunga Mitambo Yote Ya Kuchenjulia Madini Kahama

Na Greyson Mwase, Kahama

Machi 31, 2019

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mitambo yote ya kuchenjulia madini ya dhahabu Wilayani Kahama baada ya kubaini udanganyifu mkubwa kwenye uchenjuaji wa madini.

Naibu Waziri Nyongo amechukua hatua hiyo kwenye ziara yake aliyoifanya mapema leo tarehe 31 Machi, 2019 Wilayani Kahama yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini,  Ali Saidi Ali, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian, wataalam kutoka Tume ya Madini, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.

Akiwa katika ziara hiyo, alifanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group inayomilikiwa na  Theogenes Zacharia pamoja na mwenzake aliyejulikana kwa jina la  Antidius na kubaini kampuni hiyo imekuwa ikiwaibia wateja wake kupitia mfumo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Kutoka kushoto Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakishuhudia kaboni ikichomwa ili kupata dhahabu katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group tarehe 31 Machi, 2019.

Akiwa ameambatana na msafara wake mara baada ya kuwasili katika kampuni hiyo alioneshwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini waliopewa kazi maalum ya kuchunguza mfumo wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni hiyo, sehemu ya mabomba ya mfumo iliyoharibiwa kwa makusudi kwa lengo la kunasa kiasi cha dhahabu kabla ya kufikishwa katika chombo maalum cha kupokelea kwa ajili ya mteja.

Alisema kuwa, kiasi cha kaboni iliyokuwa na dhahabu iliyokamatwa ilipelekwa kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kubaini kiasi cha adhabu kilichokuwa kimeibiwa na kusisitiza kuwa baada ya kuchenjuliwa kiasi cha gramu 102 kiligundulika kutaka kuibwa.

Katika hatua nyingine mbali na kufunga mitambo ya kuchenjua madini ya dhahabu katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Kahama kuhakikisha watuhumiwa wote wa kampuni ya Ng’ana Group wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama na uchunguzi kuanza mara moja.

Katika hatua nyingine, Nyongo alisema kuwa maafisa madini wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama wataanza kufungua mtambo mmoja mmoja wa kuchenjua madini ya dhahabu mara baada ya kujiridhisha na uendeshaji wake.

Kutoka kulia, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakiangalia steel wire iliyokuwa na mabaki ya kaboni yaliyonasa, kwenye ziara yake ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group tarehe 31 Machi, 2019.

Awali akielezea siri ya wizi unaofanywa na kampuni ya Ng’ana Group, mmoja wa wateja kutoka kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Joseph Magunila & Partners, aliyepeleka kaboni kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kupata madini ya dhahabu, Wema Shibitali alisema kuwa, wakati zoezi la uchanjuaji likiendelea alishangaa kupata kiasi kidogo cha dhahabu tofauti na kaboni iliyokuwa imewekwa.

Alisimulia kuwa aliomba maafisa kutoka vyombo vya dola kufungua mfumo ili kubaini kama kuna madini yamebaki na kuongeza kuwa mara baada ya mfumo kufunguliwa walibaini kiasi kikubwa cha kaboni kilichokuwa kimebaki kwenye mfumo.

Aidha Shabitali aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwatetea wachimbaji wadogo kwa kuwa wamekuwa wakiibiwa na wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa muda mrefu.

Sehemu ya madini yaliyokamatwa katika mtambo wa kuchenjua madini unaomilikiwa na kampuni ya Ng’ana Group.

Wakati huo huo akizungumza katika msafara huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha mbali na kumpogeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea Wilaya yake na kushughulikia changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa ziara hiyo imewapa mwanga zaidi wa mbinu zinazotumiwa na wachenjuaji wa madini na kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Uchomaji wa dhahabu ukifanyika katika mtambo wa kuchenjua madini unaomilikiwa na kampuni ya Ng’ana Group.

Aliwataka wachimbaji na wachenjuaji wa madini nchini kuunga juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano pamoja na Serikali yake, Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za madini kwa kuwa waaminifu kwenye ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

Read more

Naibu Waziri Nyongo abaini udanganyifu Madini Kahama

Aelekeza soko la madini kuanzishwa mara moja………

Machi 31, 2019

Na Greyson Mwase, Kahama

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameelekeza soko la madini katika mkoa wa kimadini wa Kahama ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya Chunya, Musoma, Singida kuanzishwa mara moja ili kudhibiti utoroshwaji wa madini unaopelekea Serikali kukosa mapato yake.

Naibu Waziri Nyongo ameyasema hayo leo tarehe 31 Machi, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mjini Kahama. Wengine waliokuwepo katika mkutano huo ni pamoja na Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini,  Ali Saidi Ali, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian pamoja na wataalam kutoka Tume ya Madini.

Alisema kuwa, mara baada ya kufanya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Kahama, alibaini kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika shughuli za uchenjuaji wa madini huku akitolea mfano wa kampuni ya Busami inayojihusisha na uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Alisisitiza kuwa, alibaini kumekuwepo na udanganyifu kwenye uzito na kiwango halisi cha dhahabu kwenye madini yaliyopatikana hali inayopelekea Serikali kukosa mapato yake stahiki.

“Kwa mfano katika mtambo wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Busami tumebaini kuna udanganyifu kwenye uchenjuaji, jana baada ya kufika na kuona namna uchenjuaji wa madini unavyofanyika na kuelekeza wataalam wa madini kuchenjua upya mchanga uliokuwepo kwenye maji yaliyohifadhiwa, tulibaini kuna madini,” alisema Nyongo

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alisimamisha shughuli za uchenjuaji katika kampuni ya Busami na kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mmiliki wake.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Nyongo alielekeza wamiliki wote wa mitambo ya kuchenjulia madini ya dhahabu nchini kuhakikisha wanakuwa na mizani na mashine maalum za kupimia madini ya dhahabu zilizoidhinishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania, na biashara ya madini kufanyika katika masoko ya madini yaliyoanzishwa na kusisitiza kuwa lazima madini yajulikane yanapopelekwa na Ofisi za Madini Nchini kuhakikisha zinatuza kumbukumbu sahihi.

Wakati huo huo Naibu Waziri Nyongo aliagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kufuatilia iwapo hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya kampuni inayojihusisha na uchenjuaji wa madini ya dhahabu Wilayani Kahama ya Jema baada ya kukamatwa ikifanya udanganyifu hivi karibuni.

Read more

Soko la madini kufunguliwa Kahama

Na Greyson Mwase, Kahama

Machi 30, 2019

Ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kimadini wa Kahama inatarajia kuanzisha soko la madini mapema ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kudhibiti utoroshwaji wa madini.

Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyoifanya mapema leo tarehe 30 Machi, 2019 katika Wilaya ya Kahama lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akijadiliana jambo na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali (katikati) katika kampuni ya Busami iliyopo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali wataalam kutoka Tume ya Madini pamoja na wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mara baada ya kufanya ziara katika baadhi ya mitambo ya kuchenjua dhahabu, Nyongo alifanya kikao na wamiliki wa mitambo hiyo na kusikiliza kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.

Mara baada ya kusikiliza kero husika ikiwa ni pamoja na ya kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Abdulrahman A. Milandu kuhakikisha sehemu ya ofisi yake inatumika kama soko la madini ya dhahabu ambapo wauzaji na wanunuzi watakuwa wanafanya biashara huku serikali ikipata mapato yake, kauli ambayo ilipokelewa kwa shangwe na wafanyabiashara wa madini ya dhahabu.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kulia) akikagua mashine ya kupima dhahabu katika kampuni ya Busami iliyopo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo ya kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 30 Machi, 2019.

Aliendelea kusema kuwa kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, kunachochea utoroshwaji wa madini ya dhahabu kwakuwa inakuwa vigumu kwa wauzaji wa madini hayo kusafiri umbali mrefu hadi Geita kwa ajili ya kwenda kuuza madini hayo.

“Hapa tunataka kuhakikisha biashara ya madini inafanyika hapa hapa ili kuwarahisishia wafanyabiashara wa madini ya dhahabu huku Serikali ikipata mapato yake,” alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine, Nyongo aliutaka uongozi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali kama vile Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabenki na soko kuanza mara moja.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wamiliki wa mitambo ya kuchenjua dhahabu kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za madini kwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini.

Wakizungumza katika nyakati tofauti wamiliki wa mitambo ya kuchenjulia dhahabu walioshiriki katika kikao hicho mbali na kumpongeza Naibu Waziri Nyongo wamesema kuwa uwepo wa soko hilo utawarahisishia sana biashara ya madini kutokana na kuepukana na matapeli huku serikali ikipata mapato yake stahiki.

Walisema kabla ya uamuzi huo wamekuwa wakisafirisha madini hadi Geita kwa ajili ya kuuza hali inayopelekea baadhi yao kuuza kwa watu wasio waaminifu.

Read more