Archives for News & Events

Spika Ndugai afungua maonesho ya madini Bungeni Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, leo Mei 30, amefungua rasmi maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma na kuipongeza Wizara ya Madini kwa kuyaandaa.
Akitoa hotuba ya ufunguzi, Ndugai alimpongeza Waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki pamoja na watendaji wa Wizara, kwa juhudi kubwa za kutangaza na kulinda rasilimali ya madini hapa nchini. Alisisitiza kuwa, anatumaini juhudi hizo zitaendelezwa ili kuiwezesha sekta husika kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu.

Alisema kwamba Wizara ya Madini inalo jukumu kubwa la kuufahamisha umma kuhusu sekta husika kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari na maonesho mbalimbali.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (katikati), akiangalia aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, alipotembelea Banda la Chuo cha Madini (MRI) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu.

“Maonesho haya yamekuja wakati muafaka kwa sababu kipindi hiki nchi yetu iko katika mageuzi makubwa katika sekta ya madini; na ninyi wizara mnawajibika kuifanikisha azma hii kwa njia mbalimbali, hususan vyombo vya habari na maonesho kama haya.”

Aidha, Spika aliwataka wadau mbalimbali wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na usalama wa wafanyakazi wao na kulipa kodi za Serikali.

Kuhusu suala la uongezaji thamani madini kabla ya kuyauza, Ndugai alisema kwamba hilo ni suala muhimu sana kwa kuzingatia sera ya nchi ya kuwezesha uchumi wa viwanda. “Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutajenga viwanda ambavyo vitatoa fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.

Akizungumzia mchango wa Bunge katika kukuza sekta ya madini, alisema Bunge limekuwa makini katika kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta husika unakuwa wenye tija na manufaa kwa pande zote; yaani Serikali, Taifa na wawekezaji.
“Tuliunda Kamati mbalimbali za ufuatiliaji wa sekta ya madini. Nafurahi kuwaambia kwamba mambo yamekuwa yakiboreka siku hadi siku. Nawasihi tuendelee hivyohivyo kwa manufaa ya pande zote.”

Mjasiriamali anayejishughulisha na uongezaji thamani madini kwa kutengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali za urembo, Susie Kennedy (mwenye blauzi nyeupe), akimwonesha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, moja ya bidhaa anazotengeneza kutokana na madini; wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Kushoto ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.

Awali, akimkaribisha Spika kufungua maonesho husika; Waziri Kairuki alisema kuwa, Wizara imeandaa maonesho hayo kwa kuzingatia kuwa ni Wizara mpya hivyo inahitaji kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake; yakijumuisha dhima na dira.

“Baada ya Bunge lako tukufu kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini Namba 14 ya Mwaka 2010, kupitia marekebisho ya Sheria Namba 7 ya Mwaka 2017, Wizara yangu imekuwa na jukumu kubwa la kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo.”

Maonesho hayo ya siku tatu, yaliyoanza Mei 30 na kutarajiwa kuhitimishwa Juni Mosi; yameshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa (TCME) na Kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji na uongezaji thamani madini.

Read more

Naibu Waziri Biteko-Ukuta wa Mirerani utaweka rekodi Afrika

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Ujenzi wa Ukuta kuzunguka Migodi ya  Mirerani ni jambo la Kihistoria na kwamba linatarajiwa kuweka rekodi Barani Afrika.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo tarehe 23 Machi, wakati wa kikao cha Maandalizi ya Uzinduzi wa Ukuta huo unaotarajiwa kuzinduliwa mapema mwezi Aprili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John  Magufuli.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Issa Nchasi, (wa pili kulia) wakibadilishana jambo na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wa Ukuta wa Mirerani.

Aliongeza kuwa, ukuta huo ni jambo ambalo watanzania wamelisubiri kwa miaka mingi licha ya kuwepo kwa mapendekezo na sasa hatua zimechukuliwa na kutekelezwa.

Pia alilipongeza Jeshi kwa nidhamu kubwa ambayo limeonesha kwa ujenzi wa ukuta huo  wenye urefu wa kilomita 25.4  na ambao ujenzi wake umechukua kipindi cha miezi 3 tofauti na ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alilipongeza Jeshi kwa kazi ambayo imefanyika na kuwataka Wajumbe wa Kamati kukamilisha utekelezaji wa majukumu yote kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Simanjiro, Wizara ya Madini,  Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO – Manyara) na Wakala wa Barabara ( TANROAD)

Imeandaliwa na:
Asteria Muhozya, Mirerani
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               
Tovuti: madini.go.tz

Read more

Naibu Waziri Biteko akutana na wachimbaji madini Lugoba

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 06 Mei, 2018 amekutana na wachimbaji wa madini ya ujenzi aina ya kokoto katika eneo la Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. Mkutano huo uliohusisha Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wananchi, ulilenga kujadili changamoto katika uchimbaji madini ya ujenzi aina ya kokoto.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) akielezea shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko na wananchi wa wilaya ya Bagamoyo (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika katika eneo la Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Katika mkutano huo, Naibu Waziri Biteko alitoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wawekezaji  kuendeleza maeneo yao,  wawekezaji kutouza leseni kwa mtu mwingine pasipo kushirikisha serikali,    wawekezaji kuandaa mpango wa utoaji huduma kwa jamii pamoja na kuutekeleza na  Ofisi ya Madini ya Kanda ya Mashariki kufuatilia ahadi za wawekezaji katika huduma za jamii na kuwasilisha  ripoti mara moja.

Maelekezo mengine ni pamoja na Ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki kuwasilisha  ripoti ya athari za mazingira kabla ya Mei 20, 2018, wawekezaji kushirikiana na wananchi wanaowazunguka, kampuni zenye mgogoro na wananchi kuhakikisha zinamaliza tofauti zao na fedha za halmashauri  kutumika kwenye uwekezaji mwingine kwa ajili ya maendeleo.

Imeandaliwa na:
Asteria Muhozya, Mirerani
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               
Tovuti: madini.go.tz

Read more

Naibu Waziri wa Madini Mh. Biteko Biteko apiga marufuku bei holela madini ya ujenzi

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amepiga marufuku tabia ya wachimbaji wa madini ya ujenzi ya kushusha bei ya madini hayo kwa ajili ya kuuza kwa wingi, badala ya kufuata bei elekezi iliyowekwa na Serikali  huku wakiwalipa  vibarua kiasi kidogo cha fedha kisichoendana na kazi ngumu wanazofanya.

Naibu Waziri Biteko ameyasema hayo  mapema leo alipofanya ziara katika machimbo ya madini ya ujenzi aina ya kokoto katika eneo la Amboni mkoani Tanga lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kuzungumza na wananchi.

Mchimbaji mdogo wa madini ya kokoto Swalehe Khama akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye ziara hiyo.

Biteko alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wamiliki wa leseni kuuza madini aina ya kokoto kwa bei  ya chini na kupata faida huku wakiwalipa kiasi kidogo vibarua wanaofanya kazi ngumu ya kuponda kokoto kwa kutumia vifaa duni.

Akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa na wachimbaji madini ya kokoto Biteko alisema kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na  Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni hukakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha watanzania na kuwataka kuunda vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa na ruzuku kutoka Serikalini.

Alisema Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi  Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) imepanga mikakati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia ruzuku na ununuzi wa vifaa vya uchimbaji ili waweze kufanya kazi katika mzaingira rafiki na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa  Sekta ya Madini.

Akielezea hatua zilizofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya madini nchini alisema imeanza na kufanya marekebisho katika Sheria ya Madini na kanuni zake, kuondoa urasimu ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa.

Mponda kokoto, Husna Bakari akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) katika ziara hiyo.

Alisema pia Serikali imeanzisha Tume ya Madini itakayokuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za madini  ikiwa ni pamoja na  kusogeza huduma za utoaji wa leseni za madini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wa madini ya ujenzi kulinda rasilimali za madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Kumekuwepo na tabia ya baadhi wa wachimbaji madini kutorosha madini nje ya nchi na kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na kama Serikali tumejipanga kuhakikisha tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote,” alisisitiza Biteko.

Aidha katika hatua nyingine Biteko aliwataka wachimbaji wa madini kufuata sheria za madini pamoja na kanuni zake.

Read more

Prof. Kikula ateuliwa Mwenyekiti Tume ya Madini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Idris Suleiman Kikula kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kupitia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu tarehe 18 Aprili, 2018, ilieleza kuwa, uteuzi wa Prof. Kikula umeanza tarehe 17 Aprili, 2018. Pia, taarifa hiyo iliongeza kuwa, Rais Magufuli pia, amewateua Makamishna wa Tume hiyo ya Madini.

Tume ya Madini ilianzishwa kufuatia kupitishwa kwa Sheria Mpya ijulikanayo kama The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017 ambayo ilianza kutumika tangu tarehe 7 Julai, 2017. Aidha, Tume ya Madini imeanzishwa baada ya kufanyika Marekebisho makubwa yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 7 ya Mwaka 2017 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017, baadhi ya majukumu ya Tume ya Madini ni kama ifuatavyo;

  • Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini.
  • Kutoa Leseni za Madini.
  • Kufanya Ukaguzi wa Migodi ili kukidhi Matakwa ya Kiusalama.
  • Kutoa Vibali vya Kusafirisha Madini Ndani na Nje ya Nchi.
  • Kusimamia uchimbaji wa Madini na Sekta nzima ya Madini nchini.
  • Utatuzi wa Migogoro inayohusu Madini.

Imeandaliwa na:
Asteria Muhozya, 
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               
Tovuti: madini.go.tz

Read more

Waziri Kairuki ataka migogoro yote ya madini isuluhishwe ndani ya mwaka mmoja

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka watendaji wote wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi na kutatua migogoro yote iliyopo katika sekta husika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Ametoa maagizo hayo mapema leo, Mei 3, 2018 wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

“Lengo la Wizara ni kuhakikisha migogoro katika sekta ya madini inakwisha kabisa. Nawapongeza Naibu Mawaziri kwa kusimamia zoezi la utatuzi wa migogoro mbalimbali ambapo, mingi imekwishatatuliwa.”

Aidha, Waziri Kairuki amewaagiza watendaji na wataalam hao wa sekta ya madini, kuandaa taarifa fupi za migogoro iliyopo katika maeneo yao zikiainisha aina ya mgogoro, hatua zipi za utatuzi zimechukuliwa hadi sasa pamoja na ushauri wao kuhusu nini kifanyike ili kuhakikisha mgogoro husika unatatuliwa.

Katika hatua nyingine, pamoja na kupongeza ufanisi ulioonekana katika ukusanyaji wa maduhuli, Waziri amewataka watendaji hao kuongeza bidii na ubunifu zaidi ili kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika eneo hilo.

Amewataka kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kazi, pamoja na kuzingatia umuhimu wa dhana ya ushirikishaji majukumu mahala pa kazi, ili kupata matokeo bora zaidi.

“Kila mmoja aangalie Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unataka nini na aone jinsi gani anautekeleza katika nafasi yake,” alisisitiza.

Vilevile, amewataka kuhakikisha wanakuwa na uelewa mzuri wa sheria na kanuni mpya za madini ili waweze kuzitekeleza kikamilifu.

Kuhusu suala la usalama migodini, Waziri kairuki amewataka watendaji kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini, wananchi wanaozunguka migodi na wadau wengine kwa ujumla kuhusu namna ya kuepusha ajali katika maeneo yao.

Ameshauri na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatolewe kwa kutumia lugha rahisi ili hata wale wenye elimu ndogo waweze kuelewa.

Ufunguzi wa kikao kazi hicho cha siku tatu, umehudhuriwa pia na Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara husika Prof. Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Kamishna wa Madini na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof Shukran Manya pamoja na viongozi na wataalam mbalimbali wa Wizara hiyo.

Imeandaliwa na:
Veronica Simba, Dodoma
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
Kikuyu Avenue,
P.O Box 422,
40474 Dodoma,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             
Tovuti: madini.go.tz

Read more