Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea mafanikio ya masoko ya madini nchini tangu kuanzishwa kwake mapema Machi, 2019 kwenye Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Uwekezaji Kwenye Sekta ya Madini uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Februari, 2020.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mapema Machi, 2019 hadi Desemba, 2019, masoko hayo yameiingizia Serikali kiasi cha shilingi bilioni 58.8

Profesa Manya ameyasema hayo leo tarehe 23 Februari, 2020 kwenye Mkutano wa Kimataifa hukusu Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini unaoendelea jijini Dar es Salaam unaokutanisha wadau wa madini kutoka ndani na nje ya nchi.

Waliohudhuria katika mkutano huo wa siku mbili unaomalizika leo ni pamoja naWaziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Watendaji kutoka Tume ya Madini na Mawaziri na wawakilishiwa Mawaziri kutoka kati nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Akielezea mafanikio ya masoko 28 ya madini na vituo 25 vya ununuzi wa madini yaliyoanzishwa tangu mwezi Machi 2019hadi Desemba, 2019 Profesa Manya amesema Serikali imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 58.8

Alielezea mafanikio ya Soko la Madini la Geita, Profesa Manya amesema kabla ya uanzishwaji wa soko, kiwango cha mauzo kimeongezeka kilo 100 mwaka 2018 hadi kilo 500 kwa mwezi mwaka 2019.

Ameongeza kuwa, katika kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini iliamua kujenga ukuta wa Mirerani hali iliyopelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa tanzanite kutoka kilo 164.6 mwaka 2016hadi kilo 2,772.2 kwa mwaka 2019.

Akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye uboreshaji wa huduma zinazotolewa na masoko ya Madini, Profesa Manya amesema sambamba na kuboresha miundombinu kwenye masoko ya madini, ameongeza kuwa pia imenunua vifaa vya kupima madini na kupeleka wataalam nje ya nchi kwa ajili ya kusomea masuala ya uthaminishaji wa madini ya vito.