News & Events

Tume ya Madini yatangaza zabuni ununuzi wa maeneo yenye leseni hodhi za  madini, Desemba 19, 2019

Tume ya Madini  imetangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa maeneo  10 yenye leseni hodhi za madini  na yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yaliyopo katika maeneo ya Ngara – Kagera, Kahama- Shinyanga, Chunya- Mbeya, Bariadi na Busega – Simiyu, Morogoro, Nachingwea – Lindi ambayo awali leseni hodhi zake zilikuwa zimerudishwa Serikalini.

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 19 Desemba, 2019 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kupitia mkutano wake na waandishi wa habari  uliofanyika  jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wengine wa Tume ya Madini.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma kwenye mkutano wake wenye lengo la kutangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa maeneo 10 yenye leseni hodhi za madini tarehe 19 Desemba, 2019

Profesa Kilula alifafanua kuwa, awali mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Madini Sura Namba 123 na kanuni zake ambapo  pamoja na mambo mengine, zilizokuwa leseni  hodhi za madini ( retention licence) zilirudishwa  Serikalini .

Alisema baada ya marekebisho hayo maeneo yote 10 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa Serikalini na kuongeza kuwa, wachimbaji wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo likiwa ni kuomba leseni za uchimbaji madini.

Aliendelea kusema kuwa, baada ya uchambuzi wa kina kufanyika, Serikali kupitia  Tume ya Madini, maeneo yote 10 yaliyokuwa na leseni hodhi yatatolewa kwa zabuni na kukaribisha kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi  wenye uwezo wa fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini  na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuomba zabuni hizo.

Aliongeza kuwa, mwekezaji atakayeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo atakuwa na jukumu la kufanya kazi na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini.

Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea hatua zinazochukuliwa kwa wamiliki wa leseni  wasioendeleza maeneo yao, aliwataka wamiliki  na waombaji wote wa leseni  za utafutaji na uchimbaji wa madini  wenye mapungufu kurekebisha mapungufu  hayo ndani ya  siku 30 kuanzia sasa.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa  Shukrani Manya (kushoto) akifafanua jambo katika mkutano huo.

Alifafanua mapungufu hayo kuwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria.

Profesa Manya alitaja mapungufu mengine kuwa ni pamoja na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa.

Alifafanua kuwa mpaka sasa leseni zaidi ya 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa na zaidi ya maombi 450 ya leseni za utafutaji yana mapungufu.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa kampuni au watu binafsi walioaminiwa na Serikali na kupewa leseni lakini wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, alisema leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni ambazo zimekwishatolewa lakini hazijachukuliwa zitaandikiwa hati ya makosa na yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha alisema kuwa, maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati yenye mapungufu yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa pamoja na wachimbaji wadogo waweze kuomba maeneo hayo.

Aliendelea kusema kuwa, maombi ambayo yamekidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hayajalipiwa ada ya kuandalia leseni yataondolewa kwenye mfumo ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa tangazo la zabuni husika linapatikana katika tovuti ya Wizara ya Madini ambayo ni (www.madini.go.tz)  Tume ya Madini (www.tumemadini.go.tz) magazeti ya Habari Leo na Daily News ya tarehe 20 Desemba, 2019 pamoja na blogs na mitandao ya kijamii.

TUME YA MADINI ANDAENI UTARATIBU BIASHARA YA MADINI IFANYIKE KIKANDA – BITEKO

Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma


Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo wakati akifungua mkutano wa Wafanyabiashara wa Madini uliofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Madini Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuandaa haraka utaratibu utakaowawezesha Wafanyabiashara wa Madini nchini kufanya shughuli zao katika ngazi ya Kanda tofauti na ilivyo sasa ambapo taratibu zinawataka kufanya shughuli hizo katika Mikoa zilipotolewa leseni zao.

Aliyasema hayo Septemba 7, 2019 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao na wizara uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na  Viongozi na Wataalam wa wizara na Taasisi zilizo chini yake.

Aidha, Waziri Biteko alieleza kuwa, endapo wadau hao watafanya shughuli zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa, serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutanua wigo kuwawezesha kufanya biashara ya madini katika maeneo mengi zaidi.

Waziri Biteko alisisitiza kuhusu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ya kutaka rasilimali madini kulinufaisha taifa na watanzania  na kueleza kuwa, ndoto hiyo ndiyo iliyopelekea  kufanyika kwa mageuzi mkubwa katika Sekta ya Madini.

Alikiri kuwa, kabla ya mabadiliko hakukuwa na mfumo rasmi uliowaonesha wachimbaji kujua sehemu sahihi ya kuuzia madini yao vivyo hivyo kwa wanunuzi wa madini suala ambalo lilipelekea kuwepo vitendo vya utoroshaji madini jambo ambalo lilionekana ni la kawaida.

Waziri  Biteko aliwataka wafanyabishara hao kuyatumia masoko yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini  na kusisitiza  kuwa, serikali itaendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini na kueleza kuwa, waliobainika kufanya vitendo hivyo wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na hivyo kuwataka kuwa  chanzo  cha mabadiliko ili kuzuia vitendo vya utoroshaji madini.

‘’ Tumekutana mpaka na wakemia wanaotengeneza madini feki. Kuna wengine wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunataka chumba cha madini kiwe na hewa ya kutosha,’’ alisisitiza Biteko.

Akijibu hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabishara wa Madini ya Vito (TAMIDA) Sam Mollel, kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, Waziri Biteko aliwataka kuwa na subira wakati serikali  ikishughulikia suala hilo.

Aidha, akijibu  changamoto  ya Masonara kusimamiwa  na  wizara nyingine, Waziri Biteko  aliwataka wafayabiashara hao kuwasilisha maoni kuhusu suala hilo  kama ilivyofanyika katika kuandaa Kanuni za Masoko na kuongeza kwamba,   ‘’ Tunataka kuwa wizara ambayo inatatua matatizo’’.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisisitiza kuhusu suala la kulipa kodi kama inavyowapasa na kuwataka kuyafahamu mabadiliko yaliyofanywa katika sekta na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, aliipongeza wizara kwa kazi ya kuwalea wadau wa madini na kueleza kwamba, miaka ya nyuma mambo kwenye sekta hayakuwa yakienda vizuri.

Aidha, aliwapongeza wafanyabiashara wa madini na kueleza kuwa, hivi sasa wameanza kubadilika huku tabia ya kufanya biashara ya madini kiholela ikianza kutoweka.

‘’ Sisi Kamati tunapoona mambo yanakwenda vizuri mnaturahisishia kazi yetu’’, alisisitiza Mwenyekiti wa Kamati.

Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni jitihada za wizara  za kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini  ikiwemo kusikiliza na kutatua  changamoto kwenye sekta  ili kuwezesha biashara ya madini kufanyika katika mazingira mazuri yanayoleta tija kwa pande zote.

Aidha, sambamba na mkutano huo, imefanyika Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kubwa ikiwa ni serikali kueleza nia yake ya kukifanya Chuo Cha Madini Dodoma kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akifunga semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula alitaka mchakato wa wa kukilea Chuo hicho kutochukua muda mrefu na alikitaka kijisimamie chenyewe ndani ya muda mfupi baada ya kulelewa  na kutoa elimu bora.

Pia, alitaka kozi ya Mafundi Mchundo kuwekewa msingi mzuri.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti wa Kamati aliitaka wizara kukiongezea nguvu Kituo Cha Jimolojia Tanzania (TGC) ikiwemo bajeti ya kutosha kukiwezesha kuboresha miundombinu yake.