THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

PROFESA KIKULA AZITAKA KAMPUNI ZINAZOSHIKILIA LESENI ZA UTAFUTAJI MADINI RUANGWA KUANZA UZALISHAJI


news title here
27
Aug
2020

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wawekezaji kutozishikilia leseni zao za utafiti na uchimbaji wa madini kwani kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya Madini na kanuni zake.

Profesa Kikula alitoa agizo hilo kwenye ziara yake aliyoifanya

leo tarehe 26 Agosti, 2020 katika eneo linalotarajiwa kuanzishwa miradi wa uchimbaji na uchenjuaji madini ya kinywe (graphite) wa Kampuni ya Lindi Jumbo uliopo Kijiji cha Matambarare, Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Jeremiah Hango pamoja na Maafisa wengine kutoka Tume ya Madini Mhandisi Iddi Msakuzi, Daudi Ntalima, Dickson Joram na Mhandisi Fadhili Kitivai.

Profesa Kikula alifafanua kuwa, kupitia ziara hiyo amebaini ukiukwaji wa Sheria ya Madini ambapo wawekezaji wamekuwa wakishikilia leseni za utafutaji wa madini bila kuziendeleza kwa kipindi kirefu.

“Kitendo cha kushikilia leseni za utafutaji madini bila kuziendeleza ni makosa kisheria na ni dhahiri kuwa Serikali inakosa mapato yake stahiki”, alisisitiza Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alizitaka kampuni zote zinazomiliki leseni za utafutaji madini bila kuziendeleza kuhakikisha zinaweka mikakati ya kuziendeleza kabla Tume ya Madini haijachukua hatua ya kuwaandikia hati za makosa (default notes).

Aliendelea kusema kuwa, kwa kampuni ambazo zimeshakamilisha taratibu za tathmini kwa ajili ya ulipaji wa fidia zinatakiwa kulipa fidia hizo kwa wakati ili kuwaruhusu wazawa wa eneo husika kuendelea na shughuli za maendeleo.

“Zipo baadhi ya Kampuni ambazo zimeshakamilisha taratibu za uthaminishaji na kuwaaminisha wazawa kuwa wangewalipa mapema fidia zao ili waweze kupisha shughuli za mradi kuendelea na badala yake wameshindwa kutekeleza kwa wakati na kupelekea kuwapo kwa migogoro baina ya kampuni hizo na wazawa, tunawaagiza kuacha tabia hiyo mara moja”." alisema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alielekeza kufanyika kwamkutano maalum utakaozikutanisha kampuni zote zinazomiliki leseni za utafutaji wa madini, Tume ya Madini, TIC, Taasisi za Fedha na Benki Kuu ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto zilizopelekea miradi hiyo kukwama na kutafuta ufumbuzi mapema ili miradi hiyo iweze kuanzishwa.

Kabla ya Ziara hiyo Mwenyekiti Kikula alifanya Kikao na Watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu, kuheshimiana na kudumisha upendo baina yao ili kuwezesha utendaji kazi mzuri.

Aidha, alitoa pongezi kwa ofisi hiyo kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kuwezeshaTume ya Madini kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020.

Wakati huohuo Profesa Kikula alitembelea soko la madini la Ruangwa na kufurahishwa na mwenendo wa soko hilo ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la mauzo ya madini katika soko hilo ikilinganishwa na kipindi cha nyuma