THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

SERIKALI YAHIMIZA MABENKI KUTOA MIKOPO KWA WACHIMBAJI WA MADINI


news title here
08
Aug
2020

Serikali imezitaka benki na taasisi nyingine za fedha kukopesha wachimbaji wa madini wakubwa kwa wadogo nchini ili kukuza sekta hiyo ambayo imeanza kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa.

Akifungua mafunzo jijini Dodoma tarehe 06 Agosti 2020, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema kuwa imekuwa ndoto yake ya muda mrefu ya Tume ya Madini kukutana na mabenki kwa ajili ya mustakhabali wa wachimbaji wa madini.

“Sekta ya madini kufungamanishwa na mabenki ni hatua kubwa katika kukuza sekta hiyo ambayo ina mchango mkubwa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”, alisema Nyongo.

Waziri Nyongo alibainisha ukuaji wa haraka wa Sekta ya Madini nchini na kusema kuwa miaka michache iliyopita Sekta ya Madini ilikuwa ikichangia asilimia 1.8 kwenye pato la Taifa lakini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 5.2, aliongeza kuwa sekta hiyo inakua kwa asilimia 17.7.

Alisisitiza elimu ya biashara ya madini kuendelea kutolewa kwa mabenki ili kuwajengea uwezo wakopeshaji ili kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya madini na kuwataka kuajiri wataalaam wa madini ambao wanaweza kuchambua michanganuo ya mikopo ya uchimbaji wa madini.

“Natoa wito kwa mabenki mengine kupitishwa kwenye mafunzo ili waweze kuwakopesha wachimbaji hasa wadogo na kwa kufanya hivyo kipato chao kitaongezeka, ajira zitaongezeka na mabenki yatafanya biashara kutokana na riba”, alisema Nyongo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alisema kuwa Sekta ya Madini ni sekta muhimu katika uchumi ambayo inahitaji mitaji mikubwa katika uwekezaji wake hivyo watoa mikopo ni muhimu kuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini.

“Sekta ya madini ni biashara kama biashara nyingine inahitaji mitaji mikubwa hivyo ninyi watu wa benki inabidi mjue vizuri leseni za madini, uhai wa leseni hizo na sheria na kanuni za madini”, alisema Profesa Manya.

Aidha, Profesa Manya alisema kuwa mafunzo hayo yataondoa kusitasita kutoa mikopo kwa wachimbaji hasa wadogo baada ya kuwa na uelewa mpana kuhusu mnyororo wa madini unaohusu wachimbaji, wauzaji, vifaa vya uchimbaji na uchakataji wa madini na watoa huduma wengine katika sekta hiyo.

Profesa Manya aliyaomba mabenki mengine kujengewa uwezo na kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini kwa kuzingatia vigezo vilivyopo ikiwemo uhai wa leseni ya mchimbaji.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili, mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na Sheria na Kanuni za Madini, Jiolojia na Madini yanayopatikana nchini na Leseni za Madini.