Tanzania kwa mara nyingine imeingia katika historia kwenye biashara ya Madini ya Bati baada ya kuwa miongoni mwa nchi zilizokidhi Vigezo vya kusafirisha Madini hayo nje ya nchi. Tukio hilo la Kihistoria lilifanyika Februari 23, 2020, baada ya Serikali kuzindua rasmi Cheti cha Uhalisia kwa Madini ya 3T’s yani Tungsten, Tantulum na Tin.

Kimsingi, Cheti hicho hutolewa kwa nchi mwanachama baada ya kukidhi vigezo vilivyoainishwa ambapo katika maeneo kumi ya makubaliano, suala la Madini ni itifaki ya tano ambayo inahusu udhibiti wa uvunaji haramu wa Madini.

Taarifa zilizotolewa kwa nyakati tofauti hivi karibuni na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini akiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjilana Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, walieleza kuwa, vigezo hivyo vinalenga kuhakikisha madini hayo hayatumiki kwenye kuchochea vita na migogoro kwa nchi husika na badala yake yalenge katika kuzinuaisha nchi hizo.

Uzinduzi wa Cheti cha Uhalisia ulifanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa mbele ya hadhira ya washiriki zaidi ya 1,000 kutoka ndanina nje ya nchi waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa katika Sekta ya Madini Tanzania 2020 wakiwemo Mawaziri kutoka nchi za ICGLR, Sekretarieti ya ICGLR, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, Wadau wa Madini, Wataalamwabobezi kutoka Sekta zinazojifungamanisha na Sekta ya Madini, huku Mwamini wa Muunganiko wa Bara la Afrika kutoka nchini Kenya, Prof. Patrick Lumumba akiwa kivutio kwenye mkutano huo .

Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ulifanyika tarehe 22 hadi 23 Februari, 2020 na kutanguliwa na Maonesho ya Madini mbalimbali yanayopatikana nchini yakiwemo ya Vito, Viwandani na Nishati.

Akifunga mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu ‘’Uwekezaji na Ushirikiano Endelevu katika Sekta ya Madini,’ Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliieleza hadhira kuwa Tanzania inakuwa nchi ya nne kutimiza vigezo kwa kutoa Cheti za Uhalisi kwa madini hayo wakati wa kuyauza baada ya nchi za DRC, Rwanda na Burundi.

Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza makubaliano yote ya Nchi za Maziwa Makuu kwa lengo la kuboresha Sekta ya Madini huku akizitaka nchi wanachama kubuni maeneo mapya yatayowezesha Serikali hizo kunufaika kupitia rasilimali madini.

Vilevile, aliziasa nchi Wanachama wa ICGLR kuhakikisha mikutano hiyo inakuwa endelevu ili itumike kama njia ya kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo Afrika na kuhakikisha mikutano hiyo inazaa matunda yatakayosaidia kuipeleka mbele Sekta ya Madini.

Aliongeza kuwa, Serikali imeridhika na utendaji wa Wizara ya Madinina Tume ya Madini ambapo mafanikio ya utendaji huo yanaonekana ikiwemo kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini, kukua kwa mchango wa Sekta ya Madini, udhibiti wa utoroshaji wa madini na kueleza kuwa hali hiyo imeleta mageuzi makubwa katika sekta husika.

‘’Ndugu washiriki, mafanikio yote yaliyotokea kwenye Sekta ya Madini chanzo chake ni Bunge. Kwenye nchi zilizopo hapa, chukueni haya’’, alisema.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema mkutano huo ulilenga katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kujenga ushirikiano wa kibiashara miongoni mwa wadau, kuwasikiliza wadau na kujua namna ya kuzifanyia kazi changamoto zilizopo katika sekta husika.

Aidha, alisema kwamba, mkutano huo umetumika kutangaza mafanikio ya sekta kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ikiwemo kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa Sekta ya Madini uliofanyika Mwaka 2019 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa madini nchini.

Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akizungumza katika mkutano huo, aliipongeza Serikali kwa mabadiliko ambayo yametokea kwenye Sekta ya Madini na kuipongeza Sekretarieti ya ICGLR kwa kuweka misingi mizuri kuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na rasilimali zao ikiwemo kudhibiti migogoro inayotokana na madini hayo.

Aliwataka watanzania kutokuwa watazamaji katika kushiriki na kumiliki uchumi wa madini na kueleza kuwa, tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameweka misingiinayowapa nafasi ya kumiliki uchumi huo.

‘’ Afrika bado haina kampuni kubwa za madini zote ni za kigeni, huko nyuma tulikuwa tunaibiwa sana, Rais ameyaweka chini hayo yote na sisi bunge tukamuunga mkono,’’ alisema Spika Ndugai.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji waSeretarieti ya ICGLR, Balozi Zachary Muburi alisema kwamba, cheti hicho cha uhalisia kwa Tanzania ni ishara kwa wanunuzi wa madini hayo kuwa Tanzania sasa inao uhalali wa kuuza madini hayo nahivyo kuzitaka nchi nyingine kuiga mfanoili kuwezesha usafirishaji halali wa madini ya bati.

‘’Uzinduzi huu ni hatua kubwa ya mabadiliko.lakini sisi sote tunahitaji kupambana kwa pamojaili kulinda rasilimali zetu,’’ alisema balozi Muburi.

Muburi aliongeza kuwa, rasilimalimadini katika nchi nyingine zimekuwa chanzo cha migogoro na badala ya rasilimali hiyo kutumika kama biashara imekuwa chanzo cha kuzalisha wakimbizi.

Alizitaka nchi wanachama kuhakikisha zinaendeleza juhudi za kuhakikisha rasilimali madini zinaleta Amani Afrika badala ya kuwa chanzo cha matatizo.

‘’Tanzania imekuwa nchi kiongozi barani Afrika kuleta Amani tangu enzi za Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere. Kukiwa na amani katika nchi jirani, majirani mnaishi vizuri,’’ aliongeza Balozi Muburi.

Aidha, aliongeza kwamba sekretarieti hiyo itaendelea kuzisaidia nchi wanachama wa umoja huo kuhakikisha Sektaza Madini katika nchi hizo zinaendelea na kuwa na tija kwa nchi wanachama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mawaziri wa Nchi za Maziwa Makuu na Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Jamhuri ya Uganda alizitaka nchi wanachama kuhakikisha zinakuwa na mfumo jumuishi ambao utaweka sura moja kwa wawekezaji wote watakaowekeza katika nchi wanachama.

Alisema za nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha kwamba zinakomesha vitendo vya uhalifu na migogoro inayosababishwa na uwepo wa madini hayo.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na luninga ya AZAM, alisema kwamba Cheti hicho cha uhalisi kilichotolewa kinaonesha mnyororo mzima wa madini ya bati tangu hatua za mahali yanapochimbwa, anayechimba, mahali mtaji wa mchimbaji unapotoka, soko analouzia, anayenunua na namna yanavyosafirishwa.

Aliongeza kwamba lengo ni kuhakikisha madini hayo hayana mkono wa ufadhili kuchochea mgogoro katika nchi za maziwa makuu na hayahusishi uhalifu wowote.