Archives for News & Events

TUMEJIPANGA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA KORONA – PROFESA MANYA

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa Tume ya Madini Makao Makuu pamoja na Ofisi zilizopo chini yake zimejipanga katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya korona.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa Tume ya Madini Makao Makuu pamoja na Ofisi zilizopo chini yake zimejipanga katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya korona.

Akizungumza jijini Dodoma tarehe 20 Machi, 2020 amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu utekelezaji wa wito wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya korona.

Alisema tayari Ofisi ya Tume ya Madini imeweka vitakasa mikono pamoja na maji tiririka kwenye ofisi zake lengo likiwa ni kuwakinga watumishi wake na wadau wa madiniwanaotembelea ofisi hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na maambukizi ya korona.

Aliongeza kuwa, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zimeweka vitakasa mikono na maji tiririka na kuwataka wadau wa madini wanaotembelea ofisi hizo kuanza kuvitumia ili kujikinga na maambukizi hayo.

Alisema hatua zilizochukuliwa na Tume Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya Korona ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi titirika na sabuni, au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia vikinga pua na mdomo (masks), kuepuka kugusana, kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua na mwenye historia ya kusafiri katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine Profesa Manya aliwataka wachimbaji wa madini kuepuka mikutano isiyo ya lazima na kuepuka misongamano ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo mengine yanayotolewa na Serikali.

“Ikumbukwe kuwa hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya korona lakini kwa sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba unatumika kupunguza athari za virusi vya korona, hivyo wachimbaji wa madini wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa kwenye shughuli zao za utafutaji na uchimbaji wa madini.” alisema Profesa Manya

Aidha katika hatua nyingine, Profesa Manya amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanapunguza msongamano wa watu pamoja na kuweka maji tiririka na vitakasa mikono kwenye masoko yote ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.

Read more

KAMATI YA NISHATI NA MADINI YAPONGEZA SOKO LA MADINI DAR ES SALAAM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza uanzishwaji na utendaji wa Soko la Kimataifa la Madini la Dar es Salaam na kueleza kuwa kuanzishwa kwake kumepunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya utapeli.

Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Machi, 2020 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula kwenye majumuisho mara baada ya kamati hiyo kufanya ziara kwenye soko hilo ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye miradi inayosimamiwa na Wizara ya Madini.

Ziara hiyo ilishirikisha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Ally Maganga, wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa Soko la Madini kulikuwepo na matukio ya utapeli kwenye biashara ya madini jijini Dar es Salaam hali iliyosababisha wafanyabiashara wengi wa madini kupata hasara kubwa huku Serikali ikikosa mapato yake.

Katika hatua nyingine, Kitandula aliitaka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuendelea kuboresha soko hilo huku ikitatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wafanyabiashara wa madini wanaoendesha shughuli zao kwenye soko hilo.

Aidha, aliitaka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuwahakikishia usalama wafanyabiashara wa madini wanaosafirisha madini kutoka mikoani kwenda kwenye soko hilo.

Wakati huohuo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema kuwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye masoko ya madini lengo likiwa ni kuhakikisha yanakuwa na mchango mkubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli.

Pia Nyongo aliwapongeza wafanyabiashara wa madini kwa kuwa wazalendo na kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake kwenye utendaji wa shughuli zao.

Awali akiwasilisha taarifa yake kwa Kamati hiyo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Ally Maganga alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa soko hilo Julai 17, 2019 hadi Februari, 2020 liliweza kufanya biashara ya madini ya vito yenye uzito wa karati 4,887 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 na madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu 46.7 na thamani ya shilingi bilioni 5.06.

Aliongeza kuwa, katika kipindi husika Serikali kupitia Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 382.6 ikiwa ni tozo za mrabaha wa madini na ada ya ukaguzi.

Alisisitiza kuwa Soko la Madini limekuwa la kipekee kwa kupokea madini yanayotokea katika masoko mengine ndani ya nchi ambapo katika kipindi husika kiasi cha kilogramu 651.089 cha madini ya dhahabu kimepokelewa na wahusika kusafirisha madini hayo nje ya nchi.

Read more

SEKTA YA MADINI KUZALISHA MAMILIONEA – WAZIRI BITEKO

Waziri wa Madini DotoBiteko amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madinikwa kushirikiana na Tume ya Madini inaendelea kuhakikisha inawawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili waweze kuwa mamilionea huku Serikali ikipata mapato yake kutokana na kodi mbalimbali na kuinua Sekta ya Madini.

Waziri Biteko aliyasema hayo tarehe 12 Machi, 2020 kwenye ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika katika machimbo ya mawe ya nakshi Ntyuka, Soko la Madini Dodoma na Chuo cha Madini Dodoma (MRI) yenye lengo la kufahamu utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Alisema kuwa, ili kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini wanaendesha shughuli zao kwa faida, Serikali imeweka mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini nchini na kupunguza kodi mbalimbali.

Akielezea mikakati ya kuboresha masoko ya madini nchini yaliyoanzishwa tangu mapema Machi mwaka jana Waziri Biteko alieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kuboresha miundombinu katika masoko husika ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine za kupima madini, mizani na kusomesha wataalam katika fani ya upimaji wa madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alipongeza mgodi wa kuchimba mawe wa Ntyuka uliopo jijini Dodoma kwa kukiwezesha kikundi cha wakinamama 120 kwa kuwapatia mabaki ya mawe ambayo huyatumia kuzalisha kokoto ambazo huziuza na kujipatia kipato.

Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya kikundi cha wakinamama wanaozalisha kokoto katika eneo la Ntyuka jijini Dodoma Blandina Daudi mbali na kushukuru mgodi kwa kuwapatia mabaki ya mawe kwa ajili ya kuzalisha kokoto alieleza kuwa kupitia kazihusika wameweza kufanya maendeleo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba na kusomesha watoto.

Awali akizungumza katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati ya Madini katika Soko la Madini la Dodoma, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Laurent Bujashi alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko husika kwa kipindi cha miezi sita kabla, ukusanyaji wa mapato ulikuwa ni jumla ya shilingi milioni 118.4 ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 23.6 kwa mwezi.

Bujashi aliendelea kueleza kuwa mara baada ya kuanzishwa kwa soko la madini Mei 19, 2019 makusanyo yaliongezeka hadi kufika jumla ya shilingi milioni 486.8 kwa kipindi cha miezi sita ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 54.1 kwa mwezi na kusisitiza kuwa ongezeko hilo lilitokana na uwepo wa soko na uwazi katika biashara ya madini hususan dhahabu.

Read more

TANZANIA SASA RASMI KUUZA MADINI YA BATI NJE

Tanzania kwa mara nyingine imeingia katika historia kwenye biashara ya Madini ya Bati baada ya kuwa miongoni mwa nchi zilizokidhi Vigezo vya kusafirisha Madini hayo nje ya nchi. Tukio hilo la Kihistoria lilifanyika Februari 23, 2020, baada ya Serikali kuzindua rasmi Cheti cha Uhalisia kwa Madini ya 3T’s yani Tungsten, Tantulum na Tin.

Kimsingi, Cheti hicho hutolewa kwa nchi mwanachama baada ya kukidhi vigezo vilivyoainishwa ambapo katika maeneo kumi ya makubaliano, suala la Madini ni itifaki ya tano ambayo inahusu udhibiti wa uvunaji haramu wa Madini.

Taarifa zilizotolewa kwa nyakati tofauti hivi karibuni na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini akiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjilana Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, walieleza kuwa, vigezo hivyo vinalenga kuhakikisha madini hayo hayatumiki kwenye kuchochea vita na migogoro kwa nchi husika na badala yake yalenge katika kuzinuaisha nchi hizo.

Uzinduzi wa Cheti cha Uhalisia ulifanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa mbele ya hadhira ya washiriki zaidi ya 1,000 kutoka ndanina nje ya nchi waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa katika Sekta ya Madini Tanzania 2020 wakiwemo Mawaziri kutoka nchi za ICGLR, Sekretarieti ya ICGLR, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, Wadau wa Madini, Wataalamwabobezi kutoka Sekta zinazojifungamanisha na Sekta ya Madini, huku Mwamini wa Muunganiko wa Bara la Afrika kutoka nchini Kenya, Prof. Patrick Lumumba akiwa kivutio kwenye mkutano huo .

Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ulifanyika tarehe 22 hadi 23 Februari, 2020 na kutanguliwa na Maonesho ya Madini mbalimbali yanayopatikana nchini yakiwemo ya Vito, Viwandani na Nishati.

Akifunga mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu ‘’Uwekezaji na Ushirikiano Endelevu katika Sekta ya Madini,’ Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliieleza hadhira kuwa Tanzania inakuwa nchi ya nne kutimiza vigezo kwa kutoa Cheti za Uhalisi kwa madini hayo wakati wa kuyauza baada ya nchi za DRC, Rwanda na Burundi.

Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza makubaliano yote ya Nchi za Maziwa Makuu kwa lengo la kuboresha Sekta ya Madini huku akizitaka nchi wanachama kubuni maeneo mapya yatayowezesha Serikali hizo kunufaika kupitia rasilimali madini.

Vilevile, aliziasa nchi Wanachama wa ICGLR kuhakikisha mikutano hiyo inakuwa endelevu ili itumike kama njia ya kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo Afrika na kuhakikisha mikutano hiyo inazaa matunda yatakayosaidia kuipeleka mbele Sekta ya Madini.

Aliongeza kuwa, Serikali imeridhika na utendaji wa Wizara ya Madinina Tume ya Madini ambapo mafanikio ya utendaji huo yanaonekana ikiwemo kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini, kukua kwa mchango wa Sekta ya Madini, udhibiti wa utoroshaji wa madini na kueleza kuwa hali hiyo imeleta mageuzi makubwa katika sekta husika.

‘’Ndugu washiriki, mafanikio yote yaliyotokea kwenye Sekta ya Madini chanzo chake ni Bunge. Kwenye nchi zilizopo hapa, chukueni haya’’, alisema.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema mkutano huo ulilenga katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kujenga ushirikiano wa kibiashara miongoni mwa wadau, kuwasikiliza wadau na kujua namna ya kuzifanyia kazi changamoto zilizopo katika sekta husika.

Aidha, alisema kwamba, mkutano huo umetumika kutangaza mafanikio ya sekta kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ikiwemo kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa Sekta ya Madini uliofanyika Mwaka 2019 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa madini nchini.

Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akizungumza katika mkutano huo, aliipongeza Serikali kwa mabadiliko ambayo yametokea kwenye Sekta ya Madini na kuipongeza Sekretarieti ya ICGLR kwa kuweka misingi mizuri kuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na rasilimali zao ikiwemo kudhibiti migogoro inayotokana na madini hayo.

Aliwataka watanzania kutokuwa watazamaji katika kushiriki na kumiliki uchumi wa madini na kueleza kuwa, tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameweka misingiinayowapa nafasi ya kumiliki uchumi huo.

‘’ Afrika bado haina kampuni kubwa za madini zote ni za kigeni, huko nyuma tulikuwa tunaibiwa sana, Rais ameyaweka chini hayo yote na sisi bunge tukamuunga mkono,’’ alisema Spika Ndugai.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji waSeretarieti ya ICGLR, Balozi Zachary Muburi alisema kwamba, cheti hicho cha uhalisia kwa Tanzania ni ishara kwa wanunuzi wa madini hayo kuwa Tanzania sasa inao uhalali wa kuuza madini hayo nahivyo kuzitaka nchi nyingine kuiga mfanoili kuwezesha usafirishaji halali wa madini ya bati.

‘’Uzinduzi huu ni hatua kubwa ya mabadiliko.lakini sisi sote tunahitaji kupambana kwa pamojaili kulinda rasilimali zetu,’’ alisema balozi Muburi.

Muburi aliongeza kuwa, rasilimalimadini katika nchi nyingine zimekuwa chanzo cha migogoro na badala ya rasilimali hiyo kutumika kama biashara imekuwa chanzo cha kuzalisha wakimbizi.

Alizitaka nchi wanachama kuhakikisha zinaendeleza juhudi za kuhakikisha rasilimali madini zinaleta Amani Afrika badala ya kuwa chanzo cha matatizo.

‘’Tanzania imekuwa nchi kiongozi barani Afrika kuleta Amani tangu enzi za Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere. Kukiwa na amani katika nchi jirani, majirani mnaishi vizuri,’’ aliongeza Balozi Muburi.

Aidha, aliongeza kwamba sekretarieti hiyo itaendelea kuzisaidia nchi wanachama wa umoja huo kuhakikisha Sektaza Madini katika nchi hizo zinaendelea na kuwa na tija kwa nchi wanachama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mawaziri wa Nchi za Maziwa Makuu na Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Jamhuri ya Uganda alizitaka nchi wanachama kuhakikisha zinakuwa na mfumo jumuishi ambao utaweka sura moja kwa wawekezaji wote watakaowekeza katika nchi wanachama.

Alisema za nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha kwamba zinakomesha vitendo vya uhalifu na migogoro inayosababishwa na uwepo wa madini hayo.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na luninga ya AZAM, alisema kwamba Cheti hicho cha uhalisi kilichotolewa kinaonesha mnyororo mzima wa madini ya bati tangu hatua za mahali yanapochimbwa, anayechimba, mahali mtaji wa mchimbaji unapotoka, soko analouzia, anayenunua na namna yanavyosafirishwa.

Aliongeza kwamba lengo ni kuhakikisha madini hayo hayana mkono wa ufadhili kuchochea mgogoro katika nchi za maziwa makuu na hayahusishi uhalifu wowote.

Read more

BILIONI 66.5 ZAPATIKANA TANGU KUANZISHWA KWA MASOKO YA MADINI

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini mapema Machi mwaka jana jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 66.5 zimepatikana na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Profesa Manya ameyasema hayo leo tarehe 11 Machi, 2020 kupitia mahojiano maalum jijini Dodoma na kueleza kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madinimwezi Machi, 2019 hadi kufikia mwezi Januari, 2020 usimamizi wa masoko ya madini nchini umeendelea kuimarika ambapo, katika kipindi husika kilogramu 9,237.34 za dhahabu; karati 12,973.14 za madini ya almasi; kilogramu 20,099.17 za madini ya bati; na kilogramu 514,683.28 za madini ya vito mbalimbali ziliuzwa kupitia masoko hayo na kuipatia Serikali jumla ya shilingi bilioni66.57.

Akielezea mfano wa masoko yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuipaisha Sekta ya Madini, Profesa Manya alielezea Soko Kuu la Dhahabu Geita ambapo alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, ukusanyaji wa mapato ulikuwa wastani wa Shilingi 599,046,378.47 yaliyotokana na wastani wa mauzo ya Kilogramu 101.97 kwa mwezi kwa takwimu za kipindi cha miezi mitano kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Alisema kuwa, baada ya kuanzisha soko, makusanyo yaliongezeka hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 2.39 kwa mwezi yaliyotokana na wastani wa mauzo ya Kilogramu 360.94 zilizouzwa katika kipindi cha miezi 11 tangu soko hilo kuanzishwa Machi, 2019 hadi Januari, 2020 na kuongeza kuwa ongezeko hilo lilitokana na uwazi katika biashara ya madini ya dhahabu kwa kuwepo kwa soko hilo.

Aliongeza kuwa, kwa kipindi cha mwezi Oktoba, 2019 pekee katika Soko Kuu la Dhahabu Geita, Serikali ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kutokana na mauzo ya kilogramu 537.6 zilizouzwa

Akitolea mfano wasoko jingine la madini la Chunya lililopo Mkoani Mbeya, Profesa Manya alifafanua kuwakabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, kiasi cha wastani wa Shilingi 177,965,811.06 kilichotokana na mauzo ya dhahabu yenye uzito wa wastani wa Kilogramu 29.67 kilikuwa kikipatikanakwa mwezi kwa takwimu za kipindi cha miezi minne (4) kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Aliendelea kusema kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa Soko la Madini la Chunya mapema Mei, 2019 ndani ya kipindi cha miezi tisa Serikali ilikusanya kiasi cha wastani wa Shilingi 961,009,348.85 kilichotokana na mauzo ya dhahabu kwa wastani wa Kilogramu 176.24 kwa mwezi.

Awali akielezea uanzishwaji wa masoko ya madini 28 na vituo vya ununuzi wa madini 28 nchini Profesa Manya alisema kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kulitokana na changamoto kubwa iliyokuwa inaikabili Sekta ya Madini kwa kipindi kirefu, hasa ya utoroshaji na biashara haramu ya madini.

Akielezea manufaa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini Profesa Manya alieleza kuwa ni pamoja nakuwasaidia wachimbaji wadogo kupata huduma ya masoko naupatikanaji wa bei stahiki za madini yanayouzwa na wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uwazi katika biashara ya madini, kuimarika kwa ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli na kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini na hivyo kusaidia upatikanaji wa mapato stahiki ya Serikali kupitia tozo za mrabaha (6%) na ada ya ukaguzi (1%) za mauzo ya madini kwenye masoko.

Mafanikio mengine ni pamoja na upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo ya madini yanayozalishwa na kuuzwa na wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wadogo wa madini nchini kupitia masoko.

Read more

MASOKO YA MADINI YAINGIZA BILIONI 58.8 -PROFESA MANYA

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea mafanikio ya masoko ya madini nchini tangu kuanzishwa kwake mapema Machi, 2019 kwenye Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Uwekezaji Kwenye Sekta ya Madini uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Februari, 2020.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mapema Machi, 2019 hadi Desemba, 2019, masoko hayo yameiingizia Serikali kiasi cha shilingi bilioni 58.8

Profesa Manya ameyasema hayo leo tarehe 23 Februari, 2020 kwenye Mkutano wa Kimataifa hukusu Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini unaoendelea jijini Dar es Salaam unaokutanisha wadau wa madini kutoka ndani na nje ya nchi.

Waliohudhuria katika mkutano huo wa siku mbili unaomalizika leo ni pamoja naWaziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Watendaji kutoka Tume ya Madini na Mawaziri na wawakilishiwa Mawaziri kutoka kati nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Akielezea mafanikio ya masoko 28 ya madini na vituo 25 vya ununuzi wa madini yaliyoanzishwa tangu mwezi Machi 2019hadi Desemba, 2019 Profesa Manya amesema Serikali imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 58.8

Alielezea mafanikio ya Soko la Madini la Geita, Profesa Manya amesema kabla ya uanzishwaji wa soko, kiwango cha mauzo kimeongezeka kilo 100 mwaka 2018 hadi kilo 500 kwa mwezi mwaka 2019.

Ameongeza kuwa, katika kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini iliamua kujenga ukuta wa Mirerani hali iliyopelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa tanzanite kutoka kilo 164.6 mwaka 2016hadi kilo 2,772.2 kwa mwaka 2019.

Akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye uboreshaji wa huduma zinazotolewa na masoko ya Madini, Profesa Manya amesema sambamba na kuboresha miundombinu kwenye masoko ya madini, ameongeza kuwa pia imenunua vifaa vya kupima madini na kupeleka wataalam nje ya nchi kwa ajili ya kusomea masuala ya uthaminishaji wa madini ya vito.

Read more

MWENYEKITI TUME YA MADINI AFANYA ZIARA DODOMA

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amefanya ziara Wilayani Dodoma Mjini lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini  ya ujenzi pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano na maafisa kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.

Mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobass Katambi na kupokelewa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Michael Maganga, Profesa Kikula alianza ziara yake kwa kutembelea  kituo cha ukaguzi wa madini ujenzi cha Nala kilichopo nje ya jiji la Dodoma na kutembelea baadhi ya machimbo ya mchanga.

Akiwa katika machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na kampuni ya Tripple I General Supply Limited yaliyopo katika eneo la Mbalawala, Wilayani Dodoma Mjini mara baada ya kupokea taarifa ya uendeshaji wa shughuli zake, Profesa Kikula aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inaandaa mkataba na kusaini kati yake na wanakijiji wanaozunguka kampuni hiyo kwa ajili ya utoaji wa huduma za jamii (corporate social responsibility) na kuepuka migongano.

“Ni vyema kampuni ikahakikisha kunakuwepo na mkataba au muhtasari unaotambulika kisheria kwa ajili ya makubaliano ya maeneo ambayo kampuni itasaidia kijiji katika kipindi fulani kulingana na vipaumbele vya wananchi,” alisema Profesa Kikula.

Profesa  Kikula alisisitiza kuwa, ni vyema wananchi wakanufaika na rasilimali za madini  kwa kupata huduma za jamii kutoka kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na  shule, vituo vya afya, miundombinu, maji na kuendelea kusema kuwa kampuni inatakiwa kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa fursa ya kutoa huduma kwenye kampuni kama vile vyakula, ajira.

Awali akitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tripple I General Supply Limited,  Maglan Kipuyo alimpongeza Mwenyekiti kwa ziara yake na kusisitiza kuwa kupitia ziara zake, kero mbalimbali zimekuwa zikitatuliwa pamoja na kupewa elimu bora ya namna ya kuchimba madini ya ujenzi kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake.

Akielezea mafanikio ya kampuni yake, Kipuyo alisema tangu kuanzishwa kwa kampuni mapema mwaka huu kampuni imefanikiwa kutoa ajira zaidi ya 200, ununuzi wa mabati kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya kijiji cha Mbalawala na kuboresha miundombinu ya barabara.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na malipo ya  wastani wa shilingi milioni 15 kama mrabaha kwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kila mwezi na kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa kisima cha maji kitakachowanufaisha wanakijiji wa Mbalawala.

Aidha, Kipuyo aliongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na  kuwezesha wenye viwanda vidogo vya kufyatulia matofali mkoani Dodoma kupata mchanga.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alimtaka Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi kuhusu umuhimu wa kutoa huduma kwa jamii (corporate social responsibility) kwa wananchi wanaozunguka migodi yao kama Sheria ya Madini na kanuni zake inavyofafanua.

Profesa Kikula pia alitembelea machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na  Wema Msuya yaliyopo katika eneo la Mundemu Wilayani Dodoma Mjini na kusisitiza umuhimu wa wachimbaji wa madini ya mchanga kuchimba kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake pamoja kuzingatia suala la usalama na utunzaji wa mazingira.

“Mbali na kuchimba mchanga na kulipa mapato Serikalini ni vyema mkahakikisha suala la usalama kwenye shughuli zenu linazingatiwa na kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza,”alisema Profesa Kikula.

Naye Meneja wa machimbo hayo, Richard Tairo  mbali na kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwa kufanya ziara na kutatua changamoto mbalimbali mara moja alimhakikishia ushirikiano kati ya wachimbaji wa madini ujenzi na Serikali ili Sekta ya Madini  iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Wakati huo huo Profesa Kikula alitembelea viwanda vya kufyatulia matofali vilivyopo katika maeneo ya Vyeyula na Mlimwa C Wilayani Dodoma Mjini ili kujionea namna shughuli zinavyoendeshwa pamoja na ulipaji wa kodi Serikalini.

Profesa Kikula aliitaka Ofisi ya Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma kusimamia kwa karibu zaidi na kuwa wabunifu kwenye zoezi la ukusanyaji wa kodi mbalimbali ili  Serikali iweze kupata mapato yake stahiki.

Read more

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA UANZISHWAJI MASOKO YA MADINI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula  amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli  kutokana na kuwepo mfumo  rasmi wa mapato ya madini yanayotokana na uanzishwaji wa  masoko ya madini na Vituo Vidogo vya Ununuzi katika mikoa mbalimbali nchini.


Afisa Madini  Mkazi wa Mkoa wa Geita  Mhandisi Gabriel Mapunda (kushoto) akiwaeleza jambo Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini wakati walipotembelea soko la Madini Geita.

 Ameyasema hayo wakati kamati hiyo ilipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel  wakati wa ziara yao mkoani humo inayolenga kuangalia namna masoko ya  madini yanavyoendeshwa pamoja na kuangalia Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini  yanayoendelea mkoani humo katika Viwanja vya CCM Kalangalala.

Aidha, ameupongeza mkoa wa Geita kutokana na kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa soko la madini ikiwemo mwamko mkubwa wa wadau wa madini wanaotumia soko hilo na kueleza kuwa, soko hilo ni la mfano mzuri wa masoko huku biashara kubwa ya madini ya dhahabu inaendelea kufanyika vizuri sokoni hapo.

Ameongeza kuwa, masoko hayo yamewezesha kupatikana kwa mapato  ambayo  kabla ya kuanzishwa kwa masoko fedha nyingi zilikuwa zikipotea kutokana na tabia za utoroshaji madini  hali ambayo hivi sasa inadhibitiwa na uwepo wa masoko hayo.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti ameutaka mkoa huo kuangalia namna masuala ya Ulinzi na Usalama yanavyosimamiwa katika uendeshaji wa masoko hayo na kueleza kuwa, yapo malalamiko ambayo yametolewa ikiwemo ucheleweshaji wa muda wa kufungua masoko hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa yapo mapinduzi makubwa yaliyofanywa mkoani humo ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Sekta ya madini yakiwemo masuala yanayohusu huduma za Afya na Elimu.

Pia, ameieleza kamati hiyo kuwa, wachimbaji mkoani humo wanapata hamasa ya kuyatumia masoko hayo  hali ambayo inapelekea kupata bei halisi ya  dhahabu ikiwemo hamasa ya kuanzishwa kwa biashara  mbalimbali ambazo zimechangiwa na uwepo wa masoko.

Pia, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuhusu mpango wa mkoa huo wa kuwa na eneo rasmi la shughuli za maonesho ambayo lengo ni kufanywa Kimataifa. Mkuu wa Mkoa alisema hayo wakati akijibu hoja ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ambaye ameshauri kuhusu maonesho hayo kimataifa zaidi.

Katika  hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo ameupongeza mkoa huo kwa kuwa na soko linalongooza nchini  kwa kuzalisha na kuuza madini likifuatiwa na soko la Madini Chunya.

Naibu Waziri ameongeza kuwa, ni soko linaloongoza kwa  kukusanya mrabaha wa serikali ambapo hivi sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 2 zinakusanywa kwa mwezi sokoni hapo.

Akizungumzia mauzo ya Soko la Madini Chunya amesema hivi sasa soko hilo linauza hadi kilo 150 kutoka kilo 20 na hivyo kutumia  fursa  hiyo kuwataka wachimbaji wote na wadau wa madini nchini kuyatumia masoko hayo na kutoyaogopa.

Pia, Naibu Waziri amezuia kukamatwa kwa wadau wote wa madini wanaofuata Sheria na taratibu katika kuyatumia masoko hayo na kuwataka waachwe wafanye shughuli zao.

Akijibu hoja iliyotolewa na wadau wa madini sokoni hapo kuhusu soko hilo kufanya kazi hadi siku ya Jumapili, Naibu Waziri amesema Wizara kupitia Tume ya Madini na Mkoa wa Geita utaangalia namna ya kulifanyia kazi suala hilo na kuongeza kwamba, tayari Wizara imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya hivyo upungufu wa rasilimali watu utafanyiwa kazi

Pia, Naibu Waziri ameupongeza Mkoa huo kuwa na ubunifu wa hali ya juu  na kuulezea kuwa, unaibeba Sekta ya Madini. Pia, ameipongeza Kamati hiyo kutokana na namna inavyoishauri Wizara jambo ambalo linaiwezesha sekta kusonga mbele.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita,  Daniel Mapunda akizungumza wakati wa ziara hiyo amesema kwamba wadau wote wanapokelewa sokoni hapo ikiwemo wachimbaji wasiokuwa kwenye mfumo rasmi. Aidha, ameongeza kuwa, kwa wateja wasiojua kusoma na kuandika wanaofika katika soko la madini kwa ajili ya kupata huduma, wanasaidiwa na maafisa wa Tume ya Madini waliopo kwenye soko hilo namna zuri ya kuweka taarifa zao kwenye nyaraka mbalimbali zinazotumika kwenye ofisi hiyo.

 Mbali na Kamati hiyo kutembelea soko la Madini Geita, pia imetembelea maonesho ya madini. Aidha, katika ziara hiyo, Wajumbe hao wa Kamati wamekabidhiwa Mwongozo wa Uwekezaji wa  mkoa huo uliozinduliwa  wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo Septemba 22, 2019, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Read more