MFUMO WA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KWENYE SEKTA YA MADINI KURAHISISHA HUDUMA MIGODINI

Feb
2023
Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amesema kuwa Mfumo wa Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini utasaidia kutunza taarifa vizuri, usalama na kurahisisha shughuli za migodi
Lekashingo ameyasema hayo jijini Dodoma Februari 02, 2023 kwenye ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini kilichoshirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na wadau wa madini kutoka migodi mbalimbali nchini.
Akielezea manufaa ya mfumo huo, Lekashingo amesema kuwa utasaidia wananchi kufahamu fursa za utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini sambamba na kurahisisha utoaji na ufuatiliaji wa huduma kwa haraka.
Ameongeza kuwa mfumo utaondoa matumizi ya nakala ngumu kwenye uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuweka kumbukumbu sahihi.
Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini CPA. Venance Kasiki, ameongeza kuwa mfumo utarahisisha shughuli za migodi kufanyika kwa haraka na kupunguza ucheleweshwaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika migodini.