THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

MTAMBO WA BARUTI WA KAMPUNI YA NITRO EXPLOSIVE KUKAMILIKA MWISHONI MWA MWAKA HUU.


news title here
26
Aug
2020

Meneja Uzalishaji wa Baruti anayesimamia ujenzi wa mtambo wa kutengeneza baruti unaomilikiwa na kampuni ya Nitro Explosive, Biren Deusi amesema kuwa ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu hivyo uzalishaji wa baruti kuanza mapema Januari, 2021.

Deusi aliyasema hayo leo tarehe 21 Agosti, 2020 kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwenye kiwanda hicho Wilayani Kilwa Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake yanye lengo la kukagua shughuli za madini, kusikiliza kero mbalimbali za wachimbaji wa madini pamoja na kuzitatua katika mkoa huo.

Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Jeremiah Hango pamoja na Maafisa wengine Daudi Ntalima, Dickson Joram na Mhandisi Fadhili Kitivai.

Akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mtambo huo, Deus alifafanua kuwa, kinachosubiriwa kwa sasa ni kibali cha kuingiza mitambo hiyo kutoka Shirika la Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo taratibu za upatikanaji wa kibali hicho zinaendelea.

Alisisitiza kuwa, mara baada ya kukamilika kwa mtambo huo, utakuwa na uwezo wa kuzalisha baruti kiasi cha tani 28 kwa masaa 8 sawa na tani 84 kwa siku ambapo soko lake litakuwa ni wachimbaji wakubwa, wadogo na masoko ya nje ya nchi.

Akielezea changamoto katika utekelezaji wa ujenzi wa mtambo huo, Deus alisema kuwa ni pamoja na mlipuko wa janga la virusi vya corona lililopelekea kushindwa kuingiza baadhi ya mitambo kutoka Afrika ya Kusini na Ujerumani.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliitaka kampuni hiyo kuwasiliana na Ofisi za Tume ya Madini ili kuweza kupatiwa ushauri wa kitaalamu kwa kuzingatia Sheria ya Baruti namna ya kupangilia maeneo ya uhifadhi wa baruti katika eneo la mtambo huo ili kuweka mazingira ya utendaji kazi kuwa salama.