THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

MWENYEKITI WA TUME YA MADINI AFANYA ZIARA KATIKA OFISI YA AFISA MADINI MKAZI SIMIYU


news title here
08
Aug
2020

Tarehe 07 Agosti, 2020 Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amekutana na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu ikiwa ni sehemu za ziara yake ya siku mbili katika ofisi hiyo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto kwenye ukusanyaji wa maduhuli.

Katika ziara yake, Profesa Kikula aliambatana na Meneja Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Tume ya Madini Makao Makuu, Gift Kilimwomeshi, na watendaji wengine kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu.

Mara baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali pamoja na kuzitatua amewataka watumishi hao kufanya kazi na kuwa wabunifu na wazalendo kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili kuiwezesha Tume ya Madini kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ililopewa kwa mwaka wa fedha, 2020-2021.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuimarisha mawasiliano na mahusiano ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi.

“Mkumbuke kuwa Tume ya Madini tumeweka mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa maduhuli ambayo matunda yake yameanza kuonekana, kwa mfano kwa kipindi cha mwezi Julai tumeweza kuvuka lengo la ukusanyaji kwa mwezi husika, mawasiliano na mahusiano kwenye Ofisi za Madini ni muhimu sana kwani yanajenga timu na kuongeza ari ya kazi,” alisema Profesa Kikula.

Aidha Profesa Kikula aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa kufuata Sheria na Kanuni za Madini.

Wakizungumza katika nyakati tofauti watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, walimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Kikula pamoja na timu yake kwa kuwatembelea na kutatua changamoto pamoja na kuwaongezea ari ya kazi.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake MhandisiMchenjuaji wa Madini, EradiusErasto alisema kuwa ujio wa Profesa Kikula umeleta faraja kubwa na kujiona wa thamani sana.

Aliongeza kuwa watafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka 2020-2021 linafikiwa ili Sekta ya Madini izidi kuongeza mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Naye Fundi Sanifu Migodi, Godfrey Msumba kutoka katika ofisi hiyo aliongeza kuwa wataendeleza ushirikino na umoja uliopo kama njia mojawapo ya kuboresha mahusiano kazini.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alitembelea Soko la Madini la Simiyu lililopo kwenye Jengo la Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu na kuelekeza wafanyabiashara kuangalia namna ya kukodijengo jingine wakati wakiendelea kutumia jengo hilo kwa muda.