SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA USALAMA KWENYE USAFIRISHAJI WA MADINI KUPITIA VIWANJA VYA NDEGE
Feb
2023
Mkaguzi wa Madini kutoka Ofisi ya Tume ya Madini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Mhandisi Nyanswi Mbona amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imeendelea kuimarisha usalama kwenye usafirishaji wa madini mbalimbali kwenda nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini.
Mhandisi Mbona aliyasema hayo Februari 14, 2023 kwenye Ofisi za Tume ya Madini zilizopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwenye mahojiano maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia namna shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ya vito zinavyochangia kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.
Akielezea mchakato mzima wa usafirishaji wa madini, Mhandisi Mbona alisema kuwa mara baada ya madini kuzalishwa, kuthaminishwa na kuuzwa na kununuliwa katika masoko ya madini, madini yanayosafirishwa nje ya nchi yakiwa yamefungwa na lakiri maalum hupelekwa katika uwanja huo kwa ajili ya taratibu za usafirishwaji nje ya nchi yakiwa na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi pamoja na nyaraka nyingine muhimu za Serikali.
Alisema kuwa mara baada ya ukaguzi na kujiridhisha vibali pamoja na lakiri zilizofungwa kwenye mzigo zipo sahihi, Idara ya Forodha hutoa kibali maalum (release order) kwa ajili ya madini kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, alishauri wafanyabiashara wa madini wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine kufanya biashara kwa kuzingatia sheria ya madini pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali
Wakati huohuo alimpongeza Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo pamoja na uongozi wa Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini kupitia maelekezo mazuri ambayo wamekuwa wakitoa mara kwa mara sambamba na kutatua changamoto za wadau wa madini nchini.