THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KAHAMA WATAKIWA KUFUATA SHERIA YA MADINI NA MIONGOZO MBALIMBALI


news title here
11
Mar
2022

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timothy Ndaya amewataka wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na ujenzi katika wilaya hiyo kufuata sheria za madini pamoja na kanuni mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili uchimbaji wao uinue uchumi wa nchi bila kuleta athari zozote.

Ndaya ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini naviongozi wanaosimamia maeneo ya uchimbaji wa madini kuhusu usimamizi wa usalama, afya na mazingira kwenye migodi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga yaliyoendeshwa na Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira iliyopo chini ya Tume ya Madini yaliyofanyika Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema kuwa migogoro mingi imekuwa ikitokea katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa kuhusu sheria ya madini na kanuni zake hasa kanuni ya usalama, afya na usimamizi wa mazingira.

Ameongeza kuwa, kutokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira na uelewa mdogo wa sheria ya madinikwenye shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali kupitia Tume ya Madini imeanza kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kuepuka migogoro na ajali zinazotokea migodini.

"Ni vyema mkahakikisha mnafuata sheria na kanuni za madini, miongozo mnayopewa na Serikali na mafunzo yanayotolewa ili uchimbaji wenu ulete manufaa kwenu binafsi bila kusababisha ajali na kuleta athari kwenye mazingira," amesema Ndaya.

Katika hatua nyingine amekememea wachimbaji wadogo wanaojihusisha na wizi wa kaboni na kusisitiza kuwa Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ipo macho itawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Aidha ameshauri ujenzi wa mitambo ya kuchenjua madini katika eneo moja ili kurahisisha usimamizi wake na kupunguza athari za mazingira.

Wakati huohuo akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Henry Mditi amesema kuwa, maeneo yanayoangaziwa katika mafunzo hayo ni pamoja na usalama migodini, utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya madini usimamizi wa baruti, usimamizi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini pamoja na sheria ya madini na kanuni zake.

Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa mpanawa shughuli za migodi, sheria ya madini hivyo kupunguza matukioya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

"Kumekuwepo na changamoto ya uharibifu wa mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na ajali ndio maana tumekuwa tukiendesha mafunzo kama haya sehemu mbalimbali nchini," amesisitiza Mhandisi Mditi.

Amesisitiza kuwa mafunzo yameshatolewa katika mikoa ya kimadini ya Mirerani, Chunya, Simiyu, Singida, Dodoma na kusisitiza kuwa mafunzo

ni endelevu ambapo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini iliyobaki.

Mafunzo hayo yametolewa na wataalam ambao ni viongozi waandamizi wa Tume ya Madini wakiwa ni pamoja na Meneja wa Ukaguzi wa Migodi, Winfrida Mrema, Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Dkt. Anorld Gesase na Afisa Mazingira Mwandamizi, Abel Malulu.