WANAWAKE TUME YA MADINI WATEMBELEA KITUO CHA WASIOONA

Mar
2022
Ni kuelekea Siku ya Wanawake Duniani
Tarehe 07 Machi, 2022 wanawake kutoka Tume ya Madini wametembelea kituo cha wasioona watu wazima cha Bugiri Wilaya ya Chamwino, Dodoma na kutoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kuwatia moyo watu wazima hao.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Tume ya Madini, Kamishna wa Tume ya Madini, Jenet Lekashingo amesema kuwa ziarahiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika tarehe 08, Machi 2022 ambapo wameamua kuwakumbuka watu wazima wasioona kwa kuwapatia msaada, kuwatembelea na kuwatia moyo.
“Tunatambua kila mtu ana mahitaji mbalimbali niwapongeze sana kuja kujitegemea kwenye kituo hiki kufanya shughuli za kujiendeleza kiuchumi na kuendeleza familia,” amesema Lekashingo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha wasioona watu wazima, Yaledi Cheleso ameeleza kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 1992 ambapo mwanzilishi wake alikuwa mwalimu wa shule ya Msingi wasioona, Keneth Mwanampalila na kina jumla ya watu wazima 31 na watoto 17.
“Tunawashukuru sana kwa kututembelea katikakituo cha makazi ya wasioona tunaishi kwa kujitegemea na kuna wengine wanaoona ndio wasaidizi wetu,” amesema Mwenyekiti.
Mmoja wa wasioona wanawake , Janeth Tadei ameshukuru uongozi wa Tume ya Madini kwa jambo walilofanya la kuwapatia msaada hakika imewatia moyo sana.
“Tunafurahi sisi , tunawapokea hata kama hamna kitu mwaka 2021 wakina mama wa madini walikuja,
tunawakaribisha sana na pale mlipotoa Mungu awaongezee, salamu zetu mnapoenda Mungu awatie nguvu,”amesema Jane.