THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

WAWEKEZAJI MADINI YA RUBI WAKARIBISHWA MUNDARARA


news title here
14
Oct
2021

Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Aidan Mhando amewataka wawekezaji wa madini kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ya rubi katika eneo la Mundarara lililopo Wilayani Longido Mkoani Arusha kutokana na uwepo mkubwa wa madini hayo.

Mhando aliyasema hayo tarehe 13 Oktoba, 2021 kupitia mahojiano maalum na timu ya wanahabari kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwenye ziara iliyofanyika katika machimbo ya rubi ya Mundarara yenye lengo la kuandaa kipindi maalum chenye kuangazia namna shughuli za uchimbaji na biashara ya madini zilivyoubadilisha mji mdogo wa Mundarara.

Alisema kuwa madini ya rubi yanayopatikana kwa wingi katika machimbo ya Mundarara yanasifika kwa ubora duniani kutokana na utofauti wake na madini ya rubi yanayopatikana sehemu nyingine.

Akielezea hali ya uwekezaji katika eneo la Mundarara, alisema kuwa kumekuwepo na ongezeko la wawekezaji kwenye uchimbaji na biashara ndogo ya madini ya rubi hali iliyochochea kasi ya ukuaji wa mji mdogo wa Mundarara ikiwa ni pamoja na upanuzi wa shughuli za kiuchumi kama vile hoteli, usafiri, ufugaji na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile barabara, maji na ujenzi wa shule.

“Bado tunawakaribisha wawekezaji wengi zaidi kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ambao tunaamini watachochea ukuaji wa kasi ya maendeleo na kulifanya eneo la Mundarara kuwa kitovu cha madini hayo,” alisema Mhando.

Katika hatua nyingine akielezea mafanikio kwenye uchimbaji na biashara ya madini ya rubi, Mhando alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu madini yenye jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.5 yaliuzwa na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi milioni 400.

Akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli katika mkoa wa Arusha katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021-2022 (Julai – Septemba), Mhando alisema ofisi yake ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.1 na kuvuka lengo kwa asilimia 108 ya lengo lililowekwa la kukusanya shilingi milioni 993 kwa kipindi husika.

Aidha aliongeza kuwa, ofisi yake inaendelea kubuni vyanzo vingine vya ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa kituo cha ununuzi wa madini ya rubi katika eneo la Mundarara ambacho kitakuwa na manufaa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini huku Serikali ikipata mapato yake.

Pia aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Longido pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano mkubwa kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini katika mkoa wa Arusha.

Wakati huohuo wafanyabiashara wadogo wa madini ya rubi waliishukuru Serikali kwa usimamizi wa Sekta ya Madini kwa kuwafanya wao kuwa sehemu ya uchumi wa madini hali iliyopelekea kuendelea kupata manufaa makubwa na uchumi wao kuimarika.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa madini katika Wilaya ya Longido, Lengai Loleya alisema kuwa tangu kuanza kwa shughuli za uchimbaji na biashara ndogo ya madini ya rubi, wakazi wa Mundarara wameendelea kuneemeka ikiwa ni pamoja na kupata fedha za kufungua biashara nyingine huku wakitunza familia zao.

Loleya aliiomba Serikali kuhamasisha uwekezaji kwenye uchimbaji mkubwa wa madini ya rubi katika eneo hilo ili kuendelea kuchochea kupaa kwa uchumi wa eneo la Mundarara

Naye Afisa Tarafa ya Engarenaibo, Isaya Emanuel aliongeza manufaa mengine yaliyochangiwa na shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kuwa ni pamoja na ongezeko la wageni kutoka katika mikoa ya jirani na kupungua kwa wizi wa mifugo uliokuwepo mwanzoni kutokana na wananchi wengi kutokuwa na kipato cha uhakika.