Tume ya Madini imefanikiwa kupata kikombe cha ushindi kwenye Kundi la Nishati na Madini katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Kikombe hicho kilikabidhiwa  kwenye sherehe za ufunguzi  wa maonesho hayo na Mgeni Rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Tume ya Madini litwaa kikombe hicho mara baada ya kuzishinda Taasisi kongwe za Serikali ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyoshika nafasi ya pili na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) iliyoshika nafasi ya tatu.

Akizungumzia ushindi huo katika mahojiano maalum, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alipongeza kazi iliyofanywa na Kamati ya Maandalizi ya Maonesho iliyoshirikisha wajumbe kutoka Tume ya Madini na kampuni za madini nchini.

Katika hatua nyingine, Profesa Manya aliwataka washiriki wa maonesho hayo kuendelea kuwatumikia watanzania kwa kuchapa kazi kwa uadilifu huku wakiendelea kutoa elimu kwa umma kupitia maonesho na vyombo vya habari.

“Tunataka ifike mahali, Sekta ya Madini iwe taswira chanya kwa kiasi kikubwa kila mahali, hivyo kuchochea ongezeko la uwekezaji nchini.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya akielezea siri ya ushindi wa Tume ya Madini alisema kuwa, ni kujipanga na ubunifu wa hali ya juu kwenye uelimishaji wa umma kupitia maonesho.

Mtinya alisema Tume ya Madini ilipanga kutumia maonesho haya kama njia mojawapo ya kujibu kero mbalimbali za wachimbaji wa madini hususan wadogo na kutangaza fursa za uwekezaji.

“Maonesho haya ni sehemu ya  mikakati ya Tume ya Madini katika kuelimisha umma, tuna mikakati mingine mingi kama vile vipindi vya redio, televisheni, magazeti, blogs, mitandao ya kijamii lengo kuhakikisha watanzania wote wanakuwa na uelewa mpana wa sekta ya madini,” alisema Mtinya

Mtinya aliishukuru Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuwa mstari wa mbele katika kuyapa maonesho hayo kipaumbele kama njia mojawapo ya kuelimisha umma.