Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuyatumia kikamilifu masoko ya madini yaliyofunguliwa katika mikoa mbalimbali nchini na kujiepusha na utoroshwaji na magendo ya madini.

Ndugai ameyasema hayo leo tarehe 26 Mei, 2019 kwenye  ufunguzi wa maonesho ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma yenye lengo la kutoa uelewa zaidi kwa  wabunge na wadau mbalimbali wanaohudhuria Bunge la Bajeti linaloendelea.

Pia amesema kuwa, kupitia maonesho hayo watajifunza masuala mbalimbali ya sekta ya madini yatakayowawezesha kuishauri vizuri Serikali.

Aidha, Spika Ndugai amesema, mabadiliko mbalimbali yanayofanyika katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja kupunguza kodi na tozo mbalimbali zilizokuwepo awali ni juhudi za Serikali katika kupunguza utoroshwaji wa madini na hivyo kuifanya kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema, Maonesho hayo ni moja ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuelimisha umma ili kutoa uelewa zaidi juu ya sekta.

Naibu Waziri, Nyongo amewataka washiriki wote katika maonesho hayo kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu pamoja na kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini ili kuvutia uwekezaji.

Akitoa taarifa ya washiriki wa maonesho hayo, Nyongo amebainisha kuwa ni pamoja na taasisi Saba (7) zilizopo chini ya Wizara ya Madini, Kampuni 32 za Madini, Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA), Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), Chama cha Wachimbaji Wakubwa wa Madini (TCM), Asasi za Kiraia na Chama cha wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), pamoja na watoa huduma katika makampuni ya migodi kama vile walipuaji wa baruti.

Maonesho haya ni ya pili ikiwa ni mwendelezo wa Maonesho yaliyofanyika mwaka jana kabla  ya uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini.